Kwa mujibu wa taarifa ya awali iliyotolewa na Mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu inaeleza kuwa jumla ya Kaya 1,150 zimeathirika na takribani watu 5,600 wameathiriwa, wakati zaidi ya watu 50 wamepoteza maisha na wengine zaidi ya 80 kujeruhiwa na kupatiwa matibabu katika hospitali. Juhudi zinaendelea za kuwatafuta watu waliopotea.
Wakazi wa Hanang’ wameiambia Sauti ya Amerika kuwa utoaji wa misaada na kukarabati miundo mbinu kutaruhusu shughuli za kiuchumi kuendelea katika maeneo yaliyoathiriwa yaliyoko mlima Hanang’ ambako barabara zimejaa matope, makazi ya watu na maeneo ya kufanyia biashara kuharibiwa.
Peter Abdallah mkazi wa Hanang’ ameitaka serikali kutoa msaada kwa wananchi ambao nyumba zao zimeharibiwa, pamoja na kwa wafanyabiashara ambao maduka yao yameathiriwa.
“Tunaiambia serikali kwasababu miundombinu imeharibika kama vile maduka na biashara za watu zilizokuwa zinaendelea serikali angalau iweze kusaidia pale palipo haribiwa ili wananchi wake wawe katika hali ya kurejea katika shughuli zao za kwaida. Hakuna miundombinu yoyote kwahiyo serikali kwa namna yoyote ile inatakiwa kutoa msaada ili kuwasaidia wananchi wake waliokumbwa na janga hili maana hili ni janga la kitaifa.” Alisema Abdallah.
Mkazi mwingine wa Hanang’ Sensa Machakwa ameiambia Sauti ya Amerika kuwa changamoto kubwa iliyopo ni kwa baadhi ya wananchi kuwapata na kuwatambua ndugu zao ambao mpaka sasa hawajulikani walipo, wakati baadhi ya waathirika wakiwa wamefukiwa matope.
“Lakini zaidi sana kubwa ni kwamba watu wameshindwa kutambua ndugu zao waliopotea maana sasa wengi wamezikwa na udongo kutoka mlimani kuja huku kwenye makazi a watu ambako ni ndani ya mji.” Alisema Machakwa.
Naye Agrey Sadick mkazi wa Katesh ameielezea miundo mbinu hususani barabara za mitaa ya mji wa Katesh kuwa na chamgamoto zinazowafanya wananchi kushindwa kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.
Alisema Sadick “Miundombinu haifai kwa maana ya barabara kubwa ya Singida mpaka Arusha angalau ilifunguliwa jana hiyo hiyo ingawa ilichukua muda mrefu lakini kwa barabara ambazo ni za pembezoni mwa mji wa Katesh kwa sasa hali ni mbaya sana.”
Wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya uokoaji katika eneo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sindiga amebainisha vituo vitatu vilivyoandaliwa na serikali kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa maporomoko kuwa ni Shule ya Sekondari Ganana, Shule ya msingi Katesh, na Shule ya Msingi Dumananga ambapo waathirika wataweza kupatiwa huduma zote za kibinaadamu.
Imetayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam