UNESCO yaongeza maeneo mapya ya urithi wa dunia

Picha ya kaburi tukufu ambalo Wayahudi wanalitambua kama eneo takatifu, na Waislamu wanaliita ni msikiti wa Mtume Ibrahim

Eneo lilioko nje ya Jiji la Iran lenye jangwa, mapango ya enzi za barafu Ujerumani na bandari ya mawe huko Brazil ambayo ilijengwa kwa ajili ya kupokea meli zilizokuwa zinaleta watumwa kutoka Afrika ni vivutio vipya vya orodha ya urithi wa dunia.

Vivutio hivyo vipya vitatu vimeongezwa katika orodha ya urithi wa dunia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) .

Kamati ya urithi wa dunia ilikutana kwa wiki moja huko Krakow, Poland, ikijadili sehemu muhimu 34 za kihistoria na maeneo ya kitamaduni ilikuongeza katika orodha hiyo.

Mwaka huu katika chaguo hizo ni pamoja na mji wa zamani na kaburi la viongozi huko Hebron, ambapo UNESCO imelifanya eneo hilo kuwa ni Kumbukumbu ya urithi wa dunia wa Wapalestina na ambao uko hatarini.

Mji huo umegawanyika na uko chini ya mamlaka ya Waisraeli na Wapalestina pamoja na mji mkongwe na kaburi likiwepo upande wa Israeli. Kaburi hilo liko eneo tukufu linaloheshimiwa na Wayahudi, Waislamu na Wakiristo.

Hata hivyo Israeli inaishutumu UNESCO kwa kujaribu kuficha mahusiano ya Wayahudi na Hebron, wakati Wapalestina wanapinga na kusema Israeli inataka kukandamiza historia yao.

Eneo jingine la kihistoria ambalo UNESCO wameliongeza kwenye orodha yao ni pamoja na Hoh Xil lilioko katika jimbo la Qinghai, Uchina, eneo lenye utamaduni wa watu wa Tibet. China imeahadi kutunza mila na utamaduni wa mkoa huo wa Tibet

Lakini kampeni ya kimataifa juu ya Tibet, inayoendeshwa na kikundi cha harakati kinachokosoa uongozi wa China katika eneo hilo, kimesema UNESCO inakubali kuhamishwa kwa nguvu wafugaji wa Tibet unaofanywa na vyombo vya serikali ya China.