“Kwa kweli huu ni msaada ambao ni zawadi ya kuokoa maisha,” amesema David Beasley, mkurugenzi mpya Mmarekani wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) la Umoja wa Mataifa.
Wakati Marekani ikiwa ndio mchangiaji mkubwa katika misaada ya kibinadamu ya dharura, Rais wa Marekani Donald Trump amependekeza punguzo kubwa katika misaada ya nje- zaidi ya asilimia 30- ambapo imesababisha mtaharuki mkubwa ulimwenguni. Tangazo hilo limekuja wakati akihudhuria mkutano wa viongozi wa kundi la nchi za G20 huko Ujerumani.
“Tunapokea hatua ya Rais Trump juu ya mgogoro wa kibinadamu unaoikabili dunia, lakini alikuwa akitangaza msaada ambao Bunge la Marekani lilikuwa limeupitisha miezi kadhaa iliopita na ni uongozi wake uliochelewesha kufikisha msaada huo,” amesema mchungaji David Beckmann, rais wa taasisi ya misaada ya Kikristo yenye makao yake Washington inayojulikana kama Christian organization Bread for the World, amesema katika taarifa yake.
Jumla ya msaada wa kibinadamu uliotolewa na Marekani kwa nchi hizo nne sasa umefikia zaidi ya dola bilioni 1.8 katika mwaka huu wa fedha, shirika la misaada la Marekani USAID limesema.
Mamilioni ya watu wa Yemen, Somalia, Sudan Kusini na Nigeria wanakabiliwa na janga la njaa wakati nchi zao zikiwa katikati ya vita.
Yemen inamlipuko mkubwa kabisa wa kipindupindu, wakati nusu ya Somalia imegubikwa na ukame na takriban watu milioni 12 wanahitaji msaada wa dharura. Sudan Kusini imeingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na Nigeria inakabiliwa na machafuko ya kundi la Boko Haram ambalo limechangia kuwepo njaa nchini.
Shirika la WFP kupitia akaunti yake ya Twitter limesema mchango huo mpya wa Marekani “ umekuja wakati mwafaka ambao tayari familia nyingi kipindi hiki cha mwaka zimeishiwa kabisa akiba zao za vyakula.”
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa mapema mwaka huu lilitahadharisha kuwa msaada wa chakula ungeweza kusitishwa kwa zaidi ya watu wa Nigeria milioni moja wenye kukabiliwa na njaa kama ahadi ya jumuiya ya kimataifa kuisaidia isingetekelezwa.