Kimbunga cha tropiki ambacho kimepiga katika kisiwa cha Madagascar wiki hii kimeripotiwa kuuwa takriban watu 18 na kuwakosesha makazi maelfu wengine, ofisi ya dharura ya taifa hilo imesema Ijumaa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, kimbunga hicho kilichopewa jina Gamane, kiligonga Madagascar Jumatano na Alhamisi, wakati kikipelekea zaidi ya watu 20,000 kukoseshwa makazi.
Kulingana na idara ya kitaifa ya majanga, Gamane kiligonga nchi kavu kaskazini mwa mji wa Vohemar, uliopo kaskazini mashariki mwa Madagascar Jumatano asubuhi, kikiwa na kasi ya upepo wa kilomita 150 kwa saa.
Kando na kusababisha maafa na kuwakosesha watu makazi, kimbunga hicho pia kimeripotiwa kuharibu barabara pamoja na daraja kasakazini mwa kisiwa hicho.