Baraza hilo limetangaza matokeo hayo saa 6, baada ya zoezi la upigaji kura kumalizika, likisema kuwa Maduro, alipata asilimia 51 ya kura zilizopigwa,ikilinganishwa na mgombea wa upinzani Edmundo Gonzalez, aliyepata asilimia 44.
Kiongozi wa upinzani Maria Corina Machando, amepinga matokeo hayo, na badala yake kusema kuwa Gonzalez, alipata asilimia 70 ya kura zilizopigwa. Wakati Maduro akisherehekea ushindi wake, serikali nyingi kote katika ukanda wa Amerika zimeomba uwazi kwenye hesabu ya kura. “Tuna wasi wasi kuwa matokeo yaliyotangazwa hayaonyeshi nia ya wapiga kura wa Venezuela,” amesema waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken.
Maduro wakati akihutubia wafuasi wake mapema Jumapili ameahidi amani na usalama. Pia amekemea ukosoaji wa kimataifa, wakati akilisifu baraza la uchaguzi linaloongozwa na watu wa karibu naye, kuwa lenye hadhi ya juu, kulinganishwa na mifumo ya mataifa mengine kama Marekani.
Rais wa Chile Gabriel Boric amesema ni vigumu kuamini matokeo ya uchaguzi huo. Kupitia ukurasa wake wa X, Boric amesema kuwa watu wa Venezuela na jumuia ya kimataifa wanataka uwazi wa mchakato wa kuhasebu kura, pamoja na uthibitisho kutoka kwa waangalizi wa kimataifa.