Zaidi ya watu 10 wameripotiwa kujeruhiwa. Idadi ya majeruhi haijathibitishwa na maafisa wa afya.
Waandamanaji waliwarushia polisi mawe na kuwasha moto barabarani kuonyesha hasira zao baada ya kuzuka ripoti kwamba idara ya polisi ya DRC ilikuwa imefanya makubaliano na polisi wa Rwanda kushirikiana kiusalama ndani ya DRC.
Waandamanaji wamesema kwamba maafisa wa usalama wa Rwanda wamesababisha uharibifu wa mali ya mamilioni ya pesa na hata vifo nchini mwao katika siku zilizopita.
Waandamanaji pia wanalalamika kuhusu ongezeko la ukosefu wa usalama, wizi wa kimabavu na mauaji mjini Goma.
Taarifa za ushirikiano kati ya polisi wa Rwanda na DRC zasambaa
Taarifa za ushirikiano wa polisi wa Rwanda na DRC, zimeenea Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, baada ya Polisi wa Rwanda kusema kwamba “walikuwa wamefikia makubaliano kuruhusu polisi wa Rwanda na DRC kushirikiana katika kukabiliana na uhalifu, ugaidi, biashara ya magendo mipakani, biashara ya dawa za kulevya, biashara haramu ya fedha na ulanguzi wa silaha.”
Polisi wa Rwanda walisema hayo baada ya mkutano na mkuu wa polisi wa DRC Dieudonne Amuli Bahigwa uliofanyika Rwanda wiki iliyopita.
Mkuu wa polisi wa Rwanda, ambaye alikuwa mkuu wa idara ya upelelezi, alisema kwamba Rwanda inazingatia sana “kushirikiana na polisi wa DRC na polisi wengine katika kanda hiyo katika kuimarisha usalama Goma, mashariki mwa DRC, na kupata habari kuhusu ugaidi katika eneo hilo kama ilivyokubaliwa katika bunge la Kinshasha.”
Kufuatia maandamano ya leo mjini Goma, Bahigwa amefutilia mbali taarifa za kuwepo mkataba kati ya Rwanda na DRC, akisema kwamba hana mamlaka ya kusaini mkataba kwa niaba ya serikali za Rwanda na DRC
“Polisi wa Congo wana uwezo wa kutekeleza majukumu yake vipasavyo. Hakuna polisi wanaojiaandaa kutoka nchi nyingine, iwe Rwanda au nchi nyingine yoyote, kuja Goma.”
Afisa mkuu wa polisi wa Goma Alisa Job amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba habari zinazoenezwa ni uvumi mtupu.
“Hakuna polisi wa Rwanda au kutoka nchi nyingine wataingia kufanya kazi nchini mwetu. Polisi wa DRC wana nguvu na uwezo wa kufanya kazi. Labda maandamano ya vijana anatokana na sababu zingine.”
Jeshi la Uganda laongeza mashambulizi DRC
Wanaharakati wa kutetea haki za kiraia mjini Goma hata hivyo wanaendelea kushuku taarifa zinazotolewa na maafisa wa serikali kuhusu uvumi wa kuwepo mkataba wa usalama kati ya Rwanda na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, wakimtaka Generali Amuli kulieleza taifa walichojadiliana katika mkutano wao nchini Rwanda.
Taarifa za mkataba kati ya polisi wa Rwanda na DRC zinajiri wakati jeshi la Uganda (UPDF) linaendelea na operesheni ya kuwasaka waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) ndani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.
Uganda pia imeanza ujenzi wa barabara ndani ya DRC na imepeleka wanajesi kadhaa kwenye mpaka wa Bunagana. Barabara hiyo itajengwa kutoka Bunagana hadi Goma kupitia Rutshuru.
Wachambuzi wasema iwapo uvumi huo ni wa kweli, hatari ni kubwa
Kulingana na mchambuzi wa usalama katika eneo la Maziwa Makuu Nabende Wamoto, itakuwa ni makosa makubwa sana kwa maafisa wa usalama wa Rwanda kuingia mji wa Goma wakati kuna wanajeshi wa Uganda sehemu hiyo.
Katika mahojiano kwa njia ya simu, Nabende amesema kwamba historia ya ushirikiano kati ya maafisa wa usalama wa Rwanda na Uganda ni mbaya sana. Amesema kwamba “Inawezekana kwamba wanasema ni polisi watashirikiana na polisi wa DRC, lakini wakawa wanajeshi waliovalia sare za polisi. Wanajeshi wa Uganda na Rwanda wamepigana mara mbili ndani ya DRC na vifo vingi vilitokea. Kwa sasa, ushirikiano kati ya Uganda na Rwanda ni mbaya kiasi cha kwamba hadi mpaka kati ya nchi hizo mbili umefungwa. Halitakuwa jambo la busara kuzungumzia kwamba maafisa wa usalama wa Rwanda nao waingie DRC kwa sasa. Itakuwa makosa makubwa sana.”
Serikali ya Rwanda imekuwa ikidai kwamba Uganda inaunga mkono makundi ya waasi wenye nia ya kuuangusha utawala wa rais Paul Kagame, madai ambayo Uganda imekanusha mara nyingi.
Uganda kwa upande wake imekuwa ikidai kwamba Rwanda inaunga mkono makundi ya wapiganaji yanayojificha nchini DRC, kuvuruga utawala wa rais Yoweri Museveni, madai ambayo vile vile yamekanushwa na Rwanda.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC