Maandamano kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu juu ya utowaji mimba yafanyika kote Marekani

Waandamanaji wajitokeza Indiana kupinga uamuzi wa Mahakama kuu ya Marekani kuhusu utoaji mimba.

Maelfu na maelfu ya Wamarekani wameandamana Jumamosi siku moja baada ya Mahakama Kuu kugeuza sheria ya miaka 50, maarufu kwa jina la Roe V. Wade, inayompatia mwanamka haki ya kutoa mimba.

Waungaji mkono uwamuzi huo, wanasherehekea kwamba hivi sasa majimbo yenye kuongozwa na Warepublican yataweza kupiga marufuku utowaji mimba.

Lakini wanaopinga uamuzi huo wamejitokeza katika takriban miji yote mikubwa ya Marekani kutoa hasira zao na kulaani uwamuzi huo huku wakidai kwamba huo sio uwamuzi wa mwisho.

Kuna majimbo 13 ambayo tayari yamepanga miswada ya sheria yakisubiri uwamuzi huo kutolewa, ili kuweza kupiga marufuku utoawaji mimba kwenye majimbo hayo.

Uwamuzi ulochukuliwa na Mahakama Kuu siku ya Ijuma unafutilia mbali sheria ya kitaifa ya kuruhusu utoaji mimba na kuyapatia majimbo uhuru na mamlaka ya kuamua njia gani kufuata kuhusiana jambo hilo.

Akilihutubia taifa mara baada ya uamuzi kutangazwa, Rais Joe Biden amewataka Wamarekani kufikisha suala hilo kwenye uchaguzi ujao wa kati kati ya mhula mwezi wa Novemba, kwa kuwachagua maseneta na wabunge ambao watalinda na kutetea haki za wanawake za kuweza kujiamulia kuhusu masuala mbali mbali ya maisha yao.

"Mahakama kwa hakika imeirudisha Marekani miaka 150 nyuma. Ni siku ya huzuni kwa nchi hii, kulingana na maoni yangu, lakini haimanishi vita vimemalizika. Hebu nieleze bayana bila ya kutetereka. njia pekee ya kuhakikisha haki ya wanawake kujiamulia inalindwa ni kwa bunge kurudisha tena uwamuzi wa Roe V. Wade na kuufanya sheria ya serikali kuu," amesema rais Biden.

Bunge la Marekani lina uwezo wa kubadili uwamuzi huo kwa kupitisha sheria ya kitaifa kurudisha Roe V. Wade, lakini mswada kama huo utahitaji theluthi mbili za kura kwenye Baraza la Senate, ikiwa ni sawa na maseneta 60.

Kwa hivi sasa baraza hilo limegawiki likiwa na nusu ya maseneta kutoka chama tawala cha Demoktarik na walobaki ni Warepublican ambao wanapinga utoaji mimba.

Wanasiasa wanawake wa Marekani walaani uamuzi wa Mahakama Kuu

Wanasiasa wanawake mashuhuri wamelaani na kueleza hasira zao kutokana na uwamuzi huo unaoligawa taifa kuu la dunia juu ya suala la, ni nani mwenye uwamuzi wa mwanamke kuamua nini la kufanya kuhusu afya na mwili wao.

Makamu Rais Kamala Harris amesema wanawake ndio wenye uwamuzi wa mwisho juu ya afya yao.

"Huu ni mzozo wa huduma ya afya, tukumbuke kwamba mamilioni ya wanawake hapa Marekani watakwenda kulala bila ya kua na huduma ya afya na huduma ya ujauzito walokua nayo hadi asubuhi ya leo." Amesema Bi. Harris.

Baadhi ya wabunge wanawake, wakiwemo Veronica Escobar, Robin Kelly na Val Demings, waliungana mara moja na waandamanaji nje ya jendo la Mahakama Kuu na kueleza hasira zao dhidi ya uwamuzi huo wa kihistoria ambao wachambuzi wanasema utaweza kubadili muelekeo wa kisiasa Marekani.

"Haturudi nyuma. Hatutakubali kuchukulia kama rais wa daraja ya pili, na bila shaka hatutakubali kuchukuliwa kama mali ya mtu." amesema mbunge wa Florida Val Demingas.

Hata hivyo mbunge wa Georgia Mrepublican mhafidhina Marjorie Taylor Greene, anasema amefurahishwa na uwamuzi huo.

"Moyo wangu umejaa na furaha kwamba mahakimu wa Mahakama Kuu wamebadili Roe Versus Wade kwa uwamuzi wao mzuri. Na kwa hakika hili ni jibu kwa dua zetu na mwanzo mwema wa kufanya kazi ya kweli kwa ajili ya maisha ya Wamarekani." amesema Taylor Greene.

Viongozi wa nchi za magharibi wakosowa uamuzi wa Mahakama Kuu

Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau, kwenye ujumbe wake wa twitter ameandika kwamba "habari zinaoztokea Marekani ni za kutisha. nina waonea huruma wanawake wa Marekani ambao hivi sasa wanatarajia kupoteza haki ya yao ya kutoa mimba."

Rais Macron wa Ufaransa ameeleza uungaji mkono wake na wanawake wa Marekani, akisema "utoaji mimba ni haki msingi ya mwanamke."

Viongozi wengine wa Ulaya ni pamoja na Mawaziri Wakuu wa Hispania, Ubelgiji, Scotland pamoja na Boris Johnson wa Uingereza.

Akizungumza na waandishi habari mjini Kigali wakati wa mkutano wa Jumuia ya Madola amesema, " Ninataka kua wazi na kila mtu kwamba hiyo si mahakama yetu. Lakini ninataka kusema bayana kwamba huo uwamuzi utakua na athari kubwa kwa jinsi watu wanavyofikiria kote duniani. Mimi ninadhani ni hatua moja kubwa kurudi nyuma. Daima nimekua nikiamini kwamba mwanamke anahaki ya kujiamulia mwenyewe na nina baki na msimamo huo."

White House imsema kwamba itafanya kila iwezalo kuzuia juhudi za majimbo kuwakataza wanawake kusafiri hadi majimbo mengine ili kutoa mimba.

Rais Biden amesema, utawala wake utalinda haki ya wanawake kupata matibabu na dawa za upangaji uzazi zinazoidhinishwa na Idara ya Chakula na Dawa, FDA ambayo ni haki msingi wa kupata huduma ya afya.