Maafisa wa Gaza wanasema mashambulizi ya Israel yameua watu 19 katika mji wa Jabalia

Picha hii inaonyesha nyumba zilizoharibiwa na mashambulizi ya Israel katika kambi ya wakimbizi huko Jabalia, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, Februari 22, 2024. Picha ya Reuters

Vifaru vya Israel vimeingia ndani upande wa mashariki katika mji wa Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza mapema Jumapili, baada ya usiku wa mashambulizi makali ya anga na ardhini, na kuua watu 19 na kujeruhi wengine kadhaa, maafisa wa afya wamesema.

Jabalia ni mji wenye kambi nane kubwa sana za kihsitoria za wakimbizi huko Gaza na zinahifadhi zaidi ya watu 100,000, wengi wao wazawa wa Palestina waliofukuzwa kutoka miji na vijiji katika eneo ambalo sasa ni Israel wakati wa vita vya 1948 kati ya Israel na nchi za kiarabu vilivyosababisha kuundwa kwa taifa la Israel.

Jumamosi jioni, jeshi la Israel limesema wanajeshi wanaoendesha operesheni huko Jabalia wamelizuia kundi la Hamas, ambalo linadhibiti Gaza kurejesha uwezo wake wa kijeshi huko.

“Tuligundua katika wiki zilizopita majaribio ya Hamas ya kuimarisha uwezo wake wa kijeshi huko Jabalia. Tunaendesha operesheni huko ili kukomesha majaribio hayo,” alisema Admirali Daniel Hagari, msemaji wa jeshi la Israel katika mkutano na waandishi wa habari.

Alisema pia kwamba wanajeshi wa Israel wanaoendesha operesheni katika mji wa Gaza wa Zeitoun waliwaua wanamgambo 30 wa Palestina.