Maafisa 70 wa zamani wa Marekani wamtaka Biden kuchukua msimamo mkali dhidi ya Israel

Rais wa Marekani Joe Biden akikutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kando ya mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa mataifa mjini New York, Septemba 20, 2023. Picha ya AFP

Takriban maafisa 70 wa zamani wa Marekani, wanadiplomasia na maafisa wa jeshi Jumatano walimtaka Rais Joe Biden kuionya Israel kuhusu kukabiliwa na hatua kali ikiwa itawanyima Wapalestina haki zao za kiraia na mahitaji msingi.

Kundi la maafisa hao lilisema katika barua pepe kwa Biden “Marekani inatakiwa kuchukua hatua madhubuti” kupinga vitendo kama hivyo, “ikiwemo kuzuia msaada wa Marekani kwa Israel kwa mujibu wa sheria na sera za Marekani.”

Miongoni mwa waliosaini barua hiyo ni mabalozi wa zamani, maafisa wa wizara ya mambo ya nje waliostaafu na maafisa wa zamani wa wizara ya ulinzi, idara ya ujasusi na White House, akiwemo Anthony Lake, mshauri wa usalama wa taifa wa rais wa zamani Bill Clinton.

Barua hiyo imesisitiza hali ya kero inayoongezeka ndani ya Marekani juu ya operesheni za Israel katika Ukanda wa Gaza zilizochochewa na shambulio la wanamgambo wa Hamas la Oktoba 7 ndani ya Israel, ambapo waliua zaidi ya watu 1,200 na kushika mateka 253.

Sehemu kubwa ya Gaza imeharibiwa na takriban Wapalestina 32,000 wameuawa, kulingana na maafisa wa afya wa Gaza.

Katika barua yake, kundi hilo lilisema operesheni ya jeshi la Israel dhidi ya Hamas ilikuwa “inahitajika na inaeleweka.”

Lakini operesheni za Israel “zimekuwa zikikiuka mara kwa mara” sheria ya kimataifa inayopiga marufuku mauaji ya kiholela na matumizi ya silaha ambayo hayatofautishi wapiganaji na raia, kundi hilo lilisema.

Lakini Israel imekanusha kuwa operesheni zake zinakiuka sheria ya kimataifa.