Mwanasheria Mkuu wa Botswana Terrence Rannowane, akitangaza matokeo hayo Ijumaa, amesema kwa vile chama cha Botswana Demokratic Party, BDP, kimeshapata zaidi ya nusu ya viti vya bunge, ingawa kura zinaendelea kuhesabiwa, analazimika kumtangaza Rais Mokgweetsi Masisi kuwa mshindi na amechaguliwa kuwa rais.
Ikiwa asilimia 73 za kura zimeshahesabiwa mungano wa vyama vya upinzani wa UDC umejinyakulia viti 13 na chama cha BPF kimepata viti vitatu.
Wa-botswana walipiga kura jumatano kuwachagua wabunge 57 wa bunge la taifa na madiwani 490 wa serikali za mitaa na mgombea wa chama kinachoshinda anatajwa kuwa rais.
Chama cha BDP hivi sasa kinahitajika kufanya mageuzi ya haraka ya uchumi kuokoa uchumi wa taifa hilo lenye utulivu wa kisiasa barani afrika kutokana na kudorora kwa uchumi wake mnamo wa miaka ya hivi karibuni.