“Litafanyika haraka. Tayari tutaona katika wiki zijazo kwamba kutakuwa na kikosi cha pili,” Conille alisema katika mahojiano mjini Washington, ambako alikutana na maafisa wa White House na wizara ya mambo ya nje.
Haiti imetikiswa kwa muda mrefu na magenge ya wahalifu, lakini hali ilikuwa mbaya zaidi mwishoni mwa mwezi Februari wakati makundi yenye silaha yalipoanzisha mashambulizi ya pamoja mjini Port-au Prince, yakisema yanataka kumuondoa madarakani waziri mkuu wa wakati huo Ariel Henry.
Kundi la kwanza la maafisa wa polisi 200 wa Kenya, sehemu ya ujumbe huo unaoungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, liliwasili mwezi Juni katika juhudi za kushirikiana na polisi wa Haiti kuleta utulivu nchini humo, ambako magenge yanadhibiti takriban asilimia 80 ya mji mkuu.
Conille amekataa kutoa maelezo kuhusu ni maafisa wangapi watawasili katika awamu ijayo, akitaja sababu za usalama.
“Lakini naweza kuwahakikishia kwamba kuna mipango inafanyika kuimarisha hatua kwa hatua uwepo wa wale ambao tayari wako Haiti,”alisema.
Conille alizungumza na AFP muda mfupi baada ya kukutana na waziri wa mambo ya nje Antony Blinken kuhusu ujumbe huo, unaopewa msaada wa kifedha na vifaa na Marekani.