Maafisa wa Idara ya Uchunguzi ya Marekani FBI, Jumatano wamedhibitisha kuwa Idara hiyo ilitoa taarifa kwa mamlaka za Ufaransa kufuatia ukamataji wa wiki iliopita wa Nasir Ahmad Tawhedi , raia wa Afghanistan mwenye umri wa miaka 27 kwenye mji wa Oklahoma City, jimboni Oklahoma, akihusishwa na kupanga upigaji risasi wa halaiki kwa jina la Islamic State, wakati wa uchaguzi wa Marekani wa Novemba.
Taarifa hiyo ilipelekea kukamatwa kwa raia mwingine wa Afghanistan, mwenye umri wa miaka 22, anayehusishwa na Tawhedi, kwenye kitongoji cha mji wa Ufaransa wa Haute Garonne, maafisa wa Ufaransa wamesema. Watu wengine watatu walikamatwa awali kwenye mji huo kupitia ushirikiano wa taarifa na Marekani.
Waendesha mashitaka dhidi ya ugaidi wa Ufaransa Jumamosi wamesema kuwa washukiwa wote wanahusishwa na kundi la Islamic State, na wanashukiwa kuhusika kwenye mpango wa kufanya shambulizi kwenye uwanja wa michezo na kwenye eneo la maduka.