Shirika la habari la Reuters limechapisha baadhi ya takwimu zikionyesha jinsi uwiano wa makabila umebadilika katika baadhi ya maeneo ya kiuchumi na kijamii tangu kumalizika utawala wa watu weupe walio wachache 1994.
Watu Wenye Kipato cha Kati
Ni asilimia 20 ya wananchi wa Afrika Kusini ni wenye kipato cha kati, kati yao asilimia 50 ni Waafrika weusi, kwa mujibu wa tafiti ya 2014 iliyofanywa na Chuo Kikuu cha Cape Town na kitengo cha ufuatiliaji na tathmini katika ofisi ya rais.
Tafiti hiyo inaonyesha kuwa idadi ya watu weusi wenye kipato cha kati ni takriban milioni 2.8.
Mwaka 1993 watu weusi waliokuwa katika daraja la kipato cha kati hisabu yao ilikuwa 600,000, kwa mujibu wa tafiti iliyofanywa na Profesa wa historia Colin Bundy, ambaye aliwahi kufundisha Chuo Kikuu cha Witwatersrand na Chuo Kikuu cha London.
Idadi ya wakazi wa Afrika Kusini ilikuwa milioni 55.7 mwaka 2018 ikilinganishwa na idadi ya milioni 40.4 mwaka 1994.
Makazi
Katika kipindi cha miaka 25, serikali imetoa nyumba milioni 4.7 kwa wazee na maskini katika jamii ya watu weusi, kwa mujibu wa kitengo cha Makazi ya Raia.
Huko siku za nyuma hapakuwa na mpango wa kutoa makazi kwa watu weusi.
Ardhi
Kiasi cha asilimia 67 cha ardhi ya kilimo cha biashara kiko katika mikono ya wazungu, ukilinganisha na asilimia 87 kabla ya mwaka 1994, kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi inayofanya utafiti juu ya Umasikini, Ardhi na Kilimo.
Ukuaji wa Uchumi
Kwa upande wa uchumi, wa nchi hii ya Afrika yenye viwanda vingi zaidi, uliongezeka kwa asilimia 0.8 mwaka 2018 baada ya uchumi kudorora mwanzoni mwa nusu ya mwaka huo wakati ukame ulipotokea na kuathiri kilimo lakini pia kukatika kwa umeme katika kampuni ya umeme Eskom imeendelea kuzorotesha shughuli za uzalishaji. Ukuaji wa uchumi unatabiriwa kufikia asilimia 1.5 mwaka 2019.
Ukosefu wa Ajira
Kwa upande wa ajira iko katika kiwango cha asilimia 27, kwa mujibu wa Idara ya Takwimu ya Afrika Kusini. Ukosefu wa ajira ulikuwa asilimia 29.6 mwaka 1994, kwa mujibu wa Benki ya Dunia ikinukuu takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Watu Weusi Wanaomiliki Hisa
Hadi kufikia 2013, takriban asilimia 23 za hisa katika makampuni 100 yaliyo orodheshwa juu kabisa katika soko la hisa la Johannesburg (JSE) zilikuwa zinamilikiwa na watu weusi, JSE imesema.
Kuongezeka kwa umiliki wa hisa tangu 1994 imekuwa kupitia miradi ya kuwawezesha watu weusi kiuchumi ambao makusudio yake ni kutatua kuwa nyuma kwa watu weusi katika umiliki wakati wa utawala wa kibaguzi, na michango ya mifuko ya hifadhi ya jamii, amana na sera za maisha.
Wastani wa Umri wa Kuishi
Wastani wa umri wa kuishi ulikuwa miaka 63.4 mwaka 2017 na miaka 61.8 mwaka 1994, kwa mujibu wa Benki ya Dunia ikinukuu kitengo cha Idadi ya Watu cha Umoja wa Mataifa. Lakini hapakuwa na uchanganuzi uliotolewa juu ya wastani huo kati ya watu weusi na wazungu nchini Afrika Kusini.