Polisi wa Zimbabwe walimkamata na kumshtaki kiongozi wa upinzani Jameson Timba na zaidi ya watu wengine 70 kwa kusababisha vurugu wakati wa mkutano binafsi uliofanyika mwishoni mwa juma, wakili wake alisema Jumatatu.
Timba, ambaye alichukua uongozi wa muda wa chama cha Citizens Coalition for Change (CCC) kufuatia kujiuzulu kwa Nelson Chamisa mwezi Januari, alikamatwa pamoja na mtoto wake wa kiume.
“Walishtakiwa kwa kusababisha vurugu na kushiriki mkutano usio halali na watafikishwa mahakamani Jumanne,” wakili wa Timba Agency Gumbo ameiambia AFP.
“Polisi wanadai waliwarushia mawe na mkutano wao hawakuwa na kibali,” alisema.
Kulingana na Gumbo, kundi hilo linazuiliwa katika vituo viwili tofauti vya polisi katika mji mkuu, Harare.
Alisema pia kwenye mtandao wa X kwamba baadhi ya watu waliokamatwa, wanahitaji matibabu.