Amemtaka Abiy kuondoa wanajeshi hao katika jimbo hilo ambalo Gebremichael anadai linaendelea kushuhudia mapigano makali licha ya serikali kutangaza ushindi siku mbili zilizopita.
Kupitia mahojiano kwa njia ya simu na shirika la habari la Reuters mapema Jumatatu, kiongozi huyo wa chama cha Tigray People’s Liberation Army, TPLF, amesema kuwa bado yuko kwenye mji mkuu wa jimbo hilo wa Mekelle, licha ya serikali kudai kuuteka Jumamosi.
Ameongeza kusema kuwa kinyume na madai ya Abiy kuwa wameshinda, mapigano yanaendelea na kwamba ushindi utakuwa wao.
Gebremichael amesema pia baadhi ya wanajeshi wa Eritrea wanaosaidiana na wanajeshi wa serikali wameshikiliwa na wapiganaji wake.
Wakati huo huo, Abiy amekiambia kikao maalum cha Bunge la Ethiopia mapema leo kuwa hakuna raia hata mmoja alieuwawa kwenye mashambulio hayo yaliyoanza Novemba 4 dhidi ya vikosi vya TPLF.