Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, ametoa muda wa mwisho kwa majeshi ya jimbo la Tigray kujisalimisha au wakabiliwe na hatua za kijeshi katika mji mkuu wa jimbo hilo wa Mekele.
Katika taarifa yake iliyowalenga viongozi wa chama cha TPLF, Abiy amewasihi wapiganaji hao kujisalimisha kwa amani ndani ya saa 72, akisema kwamba safari yao imefika mwisho.
Ameendelea kusema kwamba wapiganaji hao wapo katika hali ambayo hawawezi kutoroka na kuwataka wachukue fursa hiyo ya mwisho.
Jeshi la Ethiopia limekuwa likipigana na majeshi ya Tigray tangu vita mzozo ulipozuka Novemba 4 wakati Abiy alipotuma wanajeshi wa kitaifa katika eneo hilo.
Serikali ya Ethiopia inalishutumu jeshi la Tigray kwa kushambulia kambi ya jeshi la kitaifa katika eneo la Tigray.
Mamia ya watu wameuawa na maelfu kukimbilia Sudan tangu vita hivyo vilipoanza.
Mawasiliano yamekatwa katika eneo hilo, huduma ya internet hamna kabisa na kufanya vigumu kwa waandishi wa habari kupata uthibitisho wa idadi ya vifo na ripoti za ghasia.
Jimbo la Tigray lenye maeneo tisa, liko kaskazini mwa Ethiopia.
Hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka katika eneo hilo tangu Septemba 9 baada ya viongozi wa Tigray kuandaa uchaguzi licha ya Abiy Ahmed kuahirisha uchaguzi huo kutokana na janga la virusi vya Corona.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC