Kimbunga Milton chatishia jimbo la Florida, watu milioni 1 waombwa kuondoka

Magari yaondoka huko Naples, Florida, kuelekea Miami, Oktoba 8, 2024, wakati kimbunga Milton kikitarajiwa kuingia Florida. Picha ya AFP

Kimbunga Milton kinaelekea Pwani ya Ghuba ya Florida, hapa Marekani, na kufikia dhoruba ya kiwango cha tano Jumanne, na kusababisha msongomano mkubwa wa magari na uhaba wa mafuta, huku maafisa wakiamuru zaidi ya watu milioni 1 kukimbia kabla hakijakumba eneo la Tampa Bay.

Milton, ambacho kililipuka Jumatatu na kuwa moja ya vimbunga vikali vya bahari ya Atlantiki ambavyo havijawahi kushuhudiwa, kinatarajiwa kuingia Jumatano au mapema Alhamisi, na kutishia sehemu ya pwani ya magharibi mwa Florida yenye watu wengi ambayo bado inakabaliwa na madhara ya kimbunga Helene chini ya wiki mbili zilizopita.

Meya wa Tampa Jane Castor alionya watu dhidi ya kuendesha gari wakati wa dhoruba, akiwaomba kukumbuka athari za kimbunga Helene.

“Ukiamua kubaki katika moja ya maeneo ambapo watu wameoombwa kuondoka, utakufa,” Castor alisema.