Kesi dhidi ya mtoto wa kiume wa Rais Biden yaanza upya Jumanne

  • VOA Swahili

Hunter Biden akiwasili mahakamani akiandamana na mke wake Melissa Cohen Biden, Juni 3, 2024, Wilmington, Delaware.

Mawakili wa mtoto wa kiume wa rais wa  Marekani joe Biden, Hunter Biden Jumanne wanawasilisha hoja mahakamani, kwenye ufunguzi wa kesi ya uhalifu dhidi yake, ikitarajiwa kuhusisha  ushahidi kutoka kwa wapenzi wake wa zamani na maelezo binafsi  kuhusu matatizo yake ya matumizi ya  dawa za kulevya.

Biden anakabiliwa na mashitaka matatu ya uhalifu kutokana na kununua bunduki 2018, wakati ambapo kulingana na rekodi zilizopo, alikuwa kwenye uraibu wa dawa za kulevya. Anatuhumiwa kumdanganya muuza bunduki aliyeidhinishwa na serikali kuu, kwa kusema kuwa hakuwa akitumia dawa za kulevya, kwa hiyo akamiliki bunduki kwa siku 11.

Hunter Biden aliwasili mahakamani akiandamana na mke wake, Melissa, mama yake ambaye ni mke wa rais Jill Biden, na dada yake Ashley Biden. Kesi hiyo imefunguliwa baada ya makubaliano ya awali na waendesha mashitaka ya kuahirisha kesi hiyo hadi baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kuvunjika.

Hunter amekana tuhuma dhidi yake akidai kulengwa na idara ya sheria, baada ya warepablikan kupinga makubaliano yake na waendesha mashitaka wakidai kuwa alipewa nafasi hiyo kwa kuwa ni mtoto wa rais.