Kenya yaonya mvua kubwa itaendelea kunyesha, huku idadi ya vifo kutokana na mafuriko ikifikia 228

Wakazi wakagua barabara iliyoharibiwa vibaya na mafuriko kufuatia mvua kubwa huko Kitengela, Mei 1, 2024.

Kenya Jumapili imesema kwamba idadi ya vifo kutokana na mvua kali na mafuriko ya wiki kadhaa imeongezeka hadi 228 na kuonya kuwa hakuna dalili ya afueni wakati huu.

Huku Kenya na nchi jirani ya Tanzania zikiepuka madhara makubwa ya kimbunga Hidaya ambacho nguvu zake zimepungua baada ya kufika katika nchi hizo siku ya Jumamosi, serikali mjini Nairobi imesema nchi hiyo inaendelea kukabiliwa na mvua kubwa na hatari ya mafuriko zaidi na maporomoko ya ardhi.

Huko Magharibi mwa Kenya, mto Nyando ulivunja kingo zake mapema Jumapili asubuhi, na kukikumba kituo cha polisi, shule, hospitali na soko katika mji wa Ahero katika kaunti ya Kisumu, polisi wamesema.

Hapakuwa ripoti za mara moja kuhusu maafa, lakini polisi wa eneo hilo wamesema viwango vya maji vinazidi kuongezeka na kwamba daraja kuu nje ya Kisumu kwenye barabara kuu kuelekea Nairobi lilijaa maji.

Wiki kadhaa za mvua kubwa isiyokuwa ya kawaida, ikisababishwa na upepo wa baharini wa El Nino, imesababisha maafa na uharibifu katika maeneo mengi ya Afrika Mashariki, eneo lililo katika hatari kubwa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Zaidi ya watu 400 walifariki na maelfu wengine kukoseshwa makazi yao katika nchi kadhaa huku mafuriko na maporomoko ya matope yakisomba nyumba, barabara na madaraja.