Kwa mujibu wa shirika la habari la AP, mkuu wa Idara ya kitaifa ya wanyamapori Erustus Kanga, amesema kuwa idadi kubwa ya ndovu kwenye mbuga ya Mwea ni ishara ya utunzaji bora wa wanyama hao ndani ya miongo mitatu iliyopita. “Hii ni ishara kuwa uwindaji haramu umeshuka, na kwamba ndovu wanashamiri,” Kanga ameongeza kusema.
Wataalam walianza kuhamisha ndovu 50 wiki iliopita hadi kwenye mbuga ya kitaifa ya Aberdare yenye ukubwa wa kilomita 780 mraba, na kufikia Jumatatu, tayari ndovu 44 walikuwa wamehamishwa. Wengine 6 wamepangwa kuhamishwa Jumanne. Waziri wa Utalii Rebecca Miano alikuwa miongoni mwa watu walioshuhudia uhamishaji wa ndovu watano Jumatatu. Shughuli yenyewe ilianza alfajiri ikihusisha zaidi ya wataalam 100, wakiwa na vifaa maalum kama magari na ndege.