Rais wa Russia Vladimir Putin alisaini makubaliano na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un ambayo yanajumuisha ahadi ya ulinzi wa pande zote mbili, hatua ambayo inabadili sera ya Moscow kwa Pyongyang.
Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alisema Korea Kaskazini iliipa Russia “ zana nyingi za kijeshi” huku zote China na Iran zikiiunga mkono Moscow katika vita vyake dhidi ya Ukraine.
“Tunahitaji kufahamu kwamba mataifa ya kimabavu yanashikamana zaidi na zaidi. Yanasaidiana kwa njia ambayo hatujahawi kushuhudia hapo awali,” aliuambia mjadala wa jopo wakati wa ziara rasmi mjini Ottawa.
“Wakati zinaungana mkono zaidi na zaidi, tawala za kimabavu kama Korea Kaskazini na China, Iran, Russia, basi ni muhimu zaidi kwamba tushikamane kama nchi zinazoamini uhuru na demokrasia,” alisema.
Kuongezeka kwa ushirikiano kati ya Russia na mataifa mengine ya Asia kunamaanisha kwamba ni muhimu zaidi kwa NATO kushirikiana na washirika wake katika kanda ya Asia-Pacific, alisema, na kuongeza hii ndiyo sababu viongozi kutoka Australia, Japan, New Zealand na Korea Kusini wamealikwa kwenye mkutano wa NATO wa mwezi ujao mjini Washington.