Kwa mujibu wa vyanzo vya habari nchini humo mshukiwa alikamatwa majira ya saa 11 alfajiri Ijumaa huko mkoa wa Kigoma.
Msako ulioendeshwa kwa pamoja kati ya polisi na shirika linalojihusisha na kampeni ya kuzuia ujangili la Friedkin Anti Poaching ulifanikiwa kumkatamata mtuhumiwa akiwa na bunduki moja aina ya SMG yenye risasi 98, magazini moja na mtambo wa kutengeneza gobore.
Kwa wiki mbili polisi walikuwa kwenye msako wa kumtafuta mtu huyo na hatimaye kupata fununu yupo kijiji cha Kagera, mkoani Kigoma.
Meneja wa Kanda wa Pori la Akiba la Muyowosi Kigosi, Aloyce Mganga amesema kuwa wakati anakamatwa mtuhumiwa hakuwa na nyara yeyote ya serikali.
Hata hivyo baada ya mahojiano alikiri kuhusika na mauaji ya tembo wawili katika pori hilo karibu wiki tatu zilizopita lakini pia alikiri kuwinda wanyama na kuuza nyama bila kuwa na vibali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martini Otieno hakutaka kukiri wala kukanusha habari hiyo badala yake alisema kuwa yuko kwenye ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Yussuf Masauni na kwamba atatoa taarifa baada ya kumaliza shughuli za ziara hiyo.