Mkuu wa Tume ya taifa ya uchaguzi Oda Gasinzigwa amewataja Kagame, Frank Habineza wa chama cha Democratic Green Party na mgombea huru Philippe Mpayimana kama wagombea katika uchaguzi wa tarehe 15 Julai.
Wote Habineza na Mpayimana walikuwa pia wagombea pekee walioruhusiwa kushindana na Kagame katika uchaguzi wa mwaka 2017.
Gasinzigwa alisema katika tangazo kwenye televisheni ya serikali kwamba jumla ya fomu 9 za wagombea watarajiwa zilipokelewa.
Jina la mtu maarufu ambalo halipo kwenye orodha hiyo ya muda ni Diane Rwigara, kiongozi wa vuguvugu la People Salvation ambaye aliwahi kukataliwa kugombea katika uchaguzi wa 2017.
“Badala ya kutoa taarifa ya rekodi ya uhalifu kama inavyoagizwa na tume ya uchaguzi, alitoa nakala ya hukumu ya mahakama,” Gasinzigwa alisema, na kuongeza kuwa ameshindwa pia kutoa hati inayothibitisha kuwa ana asili ya Rwanda.
“Kuhusu sharti la kupata uidhinishaji wa saini za watu 600, hakutoa angalau saini 12 kutoka wilaya nane.”
Rwigara alikataliwa kugombea mwaka 2017 kwa tuhuma za kughushi saini za wafuasi wake kwa ajili ya fomu yake.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 42 alikamatwa, na kushtakiwa kwa kughushi na kuchochea uasi na kufungwa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya kuachiliwa huru mwaka 2018.