Kauli hizo zimekuja siku chache baada ya Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge, Ngara mkoani Kagera, Severine Niwemugizi kueleza umuhimu wa Katiba mpya kuwa ndiyo kipaumbele cha kwanza cha Watanzania.
Askofu Niwemugiza alisema yeye kama kiongozi wa dini anaongozwa na maadili, haki na ukweli hivyo hajali namna wengine watakavyomchukulia.
Akifungua mkutano wa asasi za kiraia uliolenga kujadili kuhusu Katiba Mpya wiki iliyopita, Askofu Niwemugizi alisema imefika wakati nchi inahitaji kuwa na dira nzuri.
Amesema hakuna mtetezi wa haki za binadamu anayetaka nchi iingie kwenye machafuko kwani wote lengo lao ni kuchochea maendeleo, amani na utulivu.
Askofu Niwemugizi alisema kuanza kutokea kwa matukio ya kuteka watoto, vifo katika mazingira ya kutatanisha na ongezeko la watu wasiojulikana ni ishara mbaya.
"Hizi sio dalili nzuri kwa Taifa lenye afya njema. Ni vielelezo vyenye dira mbaya. Imefika wakati tukae kama Taifa tukubaliane kuwa tunataka dira njema ambayo ni Katiba."
Akizungumza Dar es Salaam Jumamosi Kadinali Pengo amesema kauli ya Askofu Niwemugizi ni maoni binafsi na si msimamo wa Kanisa Katoliki nchini.
Suala la Katiba Mpya ambalo baadhi ya wanaharakati na wanasiasa wanajaribu kuligeuza kuwa ajenda kuu kwa sasa, Kadinali Pengo alisema yeye binafsi kipaumbele chake ni kuona huduma za jamii kama zile elimu na afya zinaendelea kuboreshwa kwa kasi kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli inavyofanya.
“Mtu akiniambia priority (kipaumbele) ya Tanzania ni Katiba Mpya inabidi anithibitishie huo ukipaumbele maana siwezi kuona mtoto anakufa kwa njaa au kwa kukosa dawa eti kwa sababu ya Katiba Mpya.
Kwangu mimi Katiba ni kitu ambacho kije baadaye, si cha haraka. “Wanasiasa wasiache watoto wetu wafe kwa njaa kisa malumbano ya Katiba. Wasiache watoto wakose shule kwa sababu hela zote zimeishia kwenye malumbano juu ya Katiba,” alisisitiza Kadinali Pengo.
“Napenda kutamka moja kwa moja kwamba huo si msimamo wa Kanisa na hauwezi kuwa msimamo wa kanisa kwa sababu sisi tuna taratibu zetu za kuishauri serikali au kuzungumzia masuala ya jamii,” alisema.
Alisema kutokana na nafasi ya Uaskofu aliyonayo Askofu Niwemugizi, kauli yake inaweza kutafsiriwa kuwa ndiyo msimamo wa Kanisa Katoliki au wa Jimbo la Rulenge, Ngara lakini kimsingi kauli hiyo imekosa vigezo vya kuichukulia kama msimamo wa Kanisa au jimbo anakotoka.
Kwa upande wake Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Solczynski hakutofautiana na kauli ya Kadinali Pengo kwa kusema kuwa pamoja na kwamba Askofu Niwemugizi ana haki ya kutoa maoni yake lakini tatizo linakuja pale watu wakaposhindwa kung’amua kuwa ni maoni binafsi au ni ya Kanisa.
Alisisitiza kuwa Kanisa lina taratibu zake za kutoa maoni kwa masuala ya kijamii na kwa Serikali.