Jubilee, Nasa kuzindua ilani, zikiwaahidi Wakenya faraja

Wagombea urais Kenya, 2013 kutoka kushoto: James Ole Kiyiapi, Musalia Mudavadi, Paul Muite, Martha Karua, Raila Odinga, Mohammed Abdula Dida, Uhuru Kenyatta and Peter Kenneth.

Mapambano ya fikra za kisiasa kati ya vyama viwili vikubwa vilivyounganisha vyama mbali mbali nchini vinatarajiwa kwenda hatua ya juu zaidi wiki ijayo kuzindua ilani za vyama vyao nchini Kenya.

Wakati wagombea wote wawili Uhuru Kenyatta na hasimu wake wa kisiasa Raila Odinga watakapo zindua Ilani zao za uchaguzi na kuainisha kwa Wakenya ahadi mbalimbali wanazokusudia kuzitekeleza iwapo watachaguliwa Agosti 8, mfukuto wa siasa tayari umepamba moto.

Odinga, mgombea urais wa muungano wa upinzani, atakuwa wa kwanza kuzindua ilani ya chama cha Nasa Jumatatu katika uzinduzi ambao utatangazwa mubashara na vituo vyote vikubwa vya televisheni.

Rais Kenyatta anatarajiwa kuzindua ilani ya Chama cha Jubilee siku ya Jumatano.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari Kenya Jubilee imeahidi itaendeleza ujenzi wa reli ya SGR mpaka Naivasha. Ujenzi wa miundo mbinu inatazamiwa kuwa moja ya ahadi zake kuu katika ilani yake ya uchaguzi. Pia inatarajiwa kuwa itaendeleza programu ya umeme nchini Kenya.

Mwaka 2013, vyama vyote viwili Cord na Jubilee vilikuwa vinaonekana kuwa vinamapendekezo katika ilani zao yanayo karibia kufanana.

Lakini baadhi ya vyanzo vya habari katika chama hicho, hapo awali, vilikuwa wameeleza kuwa tarehe ya uzinduzi huo ilikuwa bado haijapangwa, na kuwa suala hilo linashughulikiwa kwa usiri mkubwa.

Baadhi ya matangazo tayari yameonyesha kile ambacho uongozi wa Raila utawafanyia wananchi wa Kenya iwapo watashinda katika baadhi ya matukio yalioonyeshwa wakati kampeni zinaendelea.

“Nasa inaahidi kuwa itazindua kilimo na kuhakikisha bei za bidhaa muhimu zinashuka,” amesema Odinga wakati akiwa huko eneo la Tharaka Nithi.

Mkuu wa kampeni ya Nasa, Musalia Mudavadi, pia amesema kuwa serikali ya Nasa itazipatia kaunti asilimia 45 ya Bajeti ya Taifa iwapo muungano wao utashinda.