Jeshi la Israel latungua kombora kutoka Yemen

Wahouthis wakiadhimisha siku walipouteka mji mkuu wa Yemen Sanaa, na kuonyesha makombora yao ya masafa marefu katika guaride ya kijeshi, Septemba 21, 2023.

Jeshi la Israel limeripoti kwamba limetungua kombora na ndege isiyokuwa na rubani iliyorushwa Ijumaa kutoka Yemen, ukiwa msururu wa mashambulizi ya hivi karibuni kutoka nchini humo kuilenga Israel katika wiki za hivi karibuni.

“Kombora lililorushwa kutoka Yemen na kuvuka mpaka hadi kwenye ardhi ya Israel limetunguliwa,” jeshi limesema katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Telegram.

Idara ya Israel inayotoa huduma za dharura imeripoti kwamba imewatibu watu kadhaa waliojeruhiwa au waliopata kiwewe kutokana na mashambulizi walipokuwa njiani kuelekea kwenye maeneo salama baada ya ving’ora vya tahadhari kulia kwa sababu ya mashambulizi ya anga kusikika katikati na kusini mwa nchi.