Kabla ya uteuzi wake, alikuwa katibu wa kudumu wa chama tawala cha PPRD. Pia ni mbunge wa taifa na Rais wa wabunge wa chama cha PPRD na mratibu wa muungano wa vyama madarakani kwenye bunge la taifa.
Ramazani Shadary aliwahi kuwa naibu waziri mkuu na waziri wa usalama katika serikali ya Joseph Kabila mwaka 2016.
Aliwahi pia kuwa gavana wa mkoa wa Maniema alikozaliwa. Kuhusu elimu yake, Shadary ana shahada ya chuo kikuu cha Lubumbashi katika sayansi ya siasa na utawala.
Ramazani Shadary yuko kwenye orodha ya viongozi wa serikali ya DRC waliowekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya kufuatia tuhuma za uvunjifu wa haki za binadamu nchini humo.
Uteuzi huo umeondoa kitendawili kilichokuwepo kwamba Rais Joseph Kabila aliyekuwa madarakani tangu mwaka 2001 angewania muhula mwengine.
Katiba ya DRC haimruhusu kabila kuwania muhula mwengine baada ya kuwania mihula miwili mwaka wa 2006 na 2011.
Mgombea huyo wa chama kilichoko madarakani ameteuliwa wakati leo ni siku ya mwisho kwa wagombea wote kuwasilisha fomu zao kwenye tume ya kitaifa ya uchaguzi.
Jina la Ramazani Shadary lilitangazwa na msemaji wa serekali, Lambert Mende katika mkutano na waandishi wa habari nchini DRC.
Wagombea walio jiorodhesha kushiriki uchaguzi wa disemba 23 ni 12 akiwemo mwanamke moja. Majina yanayotambulika zaidi ni Jean Pierre Bemba, Vital Kamerhe, Felix Thisekedi, mawaziri wakuu wa zamani Adolphe Muzito na Samy Badibanga, pamoja na Ramazani Shadary.
Mpinzani wa Rais Kabila ambaye yuko uhamishoni, Moise Katumbi amekataliwa na viongozi wa DRC kuingia nchini alipojitahidi mwishoni mwa juma lililopita kuingia kwenye eneo la mpakani kati ya Zambia na DRC, ili kuwasilisha fomu yake kwenye tume ya uchaguzi ya taifa.
Hatma ya Katumbi baada ya muda wa kupokea fomu za wagombea kwenye kiti cha urais kumalizika Jumatano hii, haijajulikana.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Patrick Nduwimana, Washington, DC