Israel yapeleka wanajeshi katika hospitali kuu ya Gaza

Wapalestina waliojeruhiwa wakifikishwa kwenye hospitali ya Nasser ya Gaza, Disemba 15, 2023. Picha ya AFP

Israel Alhamisi ilipeleka wanajeshi katika hospitali ya Gaza ambako imesema huenda mateka wanashikiliwa humo, huku madaktari wakionya kuwa kituo hicho muhimu cha kutoa matibabu kinafanya kazi katika mazingira magumu sana.

Uvamizi huo unajiri siku chache baada ya mapigano makali kati ya wanajeshi wa Israel na wanamgambo wa Hamas karibu na hospitali ya Nasser huko Khan Younis, moja ya vituo vikuu vya afya kusini mwa Gaza, na hospitali pekee ambayo bado inafanya kazi katika eneo hilo.

Israel ambayo iliwashtumu wapiganaji wa Hamas kwa kutumia hospitali hiyo kwa madhumuni ya kijeshi ilisema ilifanya “operesheni ya kitaalam na ya muda mfupi” kwenye kituo hicho bila kulazimisha wagonjwa na wafanyakazi kuondoka.

Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari alisema kulikuwa na taarifa za kuaminika za kijasusi kutoka kwa vyanzo mbalimbali, wakiwemo mateka walioachiwa huru, zikibaini kuwa Hamas ilishikilia mateka katika hospitali ya Nasser huko Khan Younis na kwamba huenda kuna maiti za mateka ndani ya hospitali hiyo.

Wizara ya afya huko Gaza ilio chini ya utawala wa Hamas iliripoti kwamba maelfu ya watu ambao walitafuta hifadhi katika jengo hilo, wakiwemo wagonjwa, walilazimika kuondoka katika siku za karibuni.