Israel yaishambulia Gaza licha ya onyo la Marekani na Umoja wa mataifa

Moshi watanda kufuatia mashambulizi ya Israel huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza, Mei 9, 2024. Picha ya AFP

Israel imeishambulia Gaza Jumamosi baada ya Marekani kuikosoa tena jinsi inavyoendesha vita huku Umoja wa Mataifa ukionya kuwa janga baya linaweza kutokea ikiwa Israel itauvamia mji wa Rafah wenye msongamano mkubwa.

Waandishi wa habari wa AFP wameripoti mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya eneo la pwani, ambako Umoja wa Mataifa unasema misaada imezuiliwa baada ya wanajeshi wa Israel kukaidi upinzani wa kimataifa na kuingia mashariki mwa Rafah wiki hii, na kufunga vivuko viwili.

Ripoti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliyosubiriwa kwa muda mrefu ilisema siku ya Ijumaa kwamba huenda Israel ilikiuka sheria za kimataifa katika matumizi yake ya silaha kutoka Marekani, mfadhili wake mkuu wa kijeshi, lakini haikupata ushahidi wa kutosha ili kuzuia usafirishaji wa vifaa vya kijeshi kwa Israel.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani iliwasilisha ripoti yake siku mbili baada ya Rais Joe Biden kutishia hadharani kwamba atazuia baadhi ya mabomu na silaha ikiwa Israel itaendelea na mpango wake wa kila aina ya mashambulizi dhidi ya Rafah, ambako Umoja wa Mataifa umesema watu milioni 1.4 walikimbilia huko kutafuta hifadhi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema Ijumaa kwamba Gaza inaweza kukabiliwa na “janga baya la kibinadamu” ikiwa Israel itaanzisha operesheni kamili huko Rafah.