Shirika la Kimataifa la Fedha, IMF, limesema huenda likasitisha ufadhili wake kwa Somalia katika muda wa miezi mitatu ijayo iwapo uchaguzi utacheleweshwa zaidi.
Malipo muhimu ya mishahara ya wanajeshi pia yanaweza kusitishwa.
Kulingana na mkuu wa IMF nchini Somalia Laura Jaramillo, mpango wa kusamehewa madeni ya Somalia unastahili kufanyiwa tathmini na serikali mpya kufikia May 17.
Mpango huo utapelekea deni la Somalia kupungua kutoka dola bilioni 5.2 hadi dola milioni 560.
Katika awamu ya kwanza ya mpango huo, deni hilo lilipunguzwa hadi dola bilioni 3.7 mwaka 2020.
Inatarajiwa kwamba hatua ya kupunguza deni, itaruhusu serikali kuvutia ufadhili zaidi kutoka kwa washirika wa kimataifa ili kujenga sekta binafsi.
Uchaguzi wa Somalia ulikuwa umepangwa kufanyika Novemba mwaka 2020 lakini umeahirishwa mara mbili kutokana na hali ya kutoelewana kuhusu namna ya kuendesha uchaguzi huo.