IGAD inaonya Sudan Kusini 'inaweza kurudi katika vita'

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir (kulia) na Makamu wa Rais Riek Machar(kushoto), wakihudhuria ibada ya misa iliyoongozwa na Papa Francis huko Juba, Februari 5, 2023. Picha ya AP

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir (kulia) na Makamu wa Rais Riek Machar(kushoto), wakihudhuria ibada ya misa iliyoongozwa na Papa Francis huko Juba, Februari 5, 2023. Picha ya AP

Jumuia ya maendeleo ya Afrika Mashariki Jumatano ilionya kwamba mapigano ya hivi karibuni nchini Sudan Kusini yanaipeleka nchi hiyo “kwenye hatari ya kurudi katika vita.”

Kupitia historia yake fupi, taifa hilo maskini limekumbwa na na mzozo wa kisiasa na ukosefu wa usalama, lakini wasiwasi uliongezeka hivi karibuni baada ya mapigano kati ya majeshi washirika kwa viongozi hasimu wa nchi hiyo.

Rais Salva Kiir aliapa kwamba nchi haiwezi kurejea katika vita, lakini mapigano hayo yalitishia makubaliano ya 2018 ya kushirikiana madaraka ambayo yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano kati yake na Makamu wa kwanza wa Rais Riek Machar.

IGAD ilisema ghasia hizo ni za hivi karibuni katika msururu wa matukio “yanayoipeleka Sudan Kusini kwenye hatari ya kurudi katika vita”.

Jumapili, Marekani iliamuru wafanyakazi wote wasio wa muhimu nchini humo kuondoka, ikionya kuhusu“ mzozo wa silaha unaoendelea”.

Mkuu wa jeshi la Uganda Jumanne alitangaza kwamba vikosi maalum vya nchi hiyo vilipelekwa huko Juba kuisaidia serikali.