Idadi ya vifo kutokana na COVID-19 yavuka milioni nchini Marekani

FILE - Rais wa Marekani Joe Biden akizungumza katika mkutano wa COVID-19, White House mjini Washington, Sept. 22, 2021.

White House inasema, idadi ya vifo kutokana na COVID-19 hapa Marekani, imevuka na kuwa zaidi ya milioni. Rais wa Marekani amesema nchi imefikia “ hatua ya kusikitisha” na kila kifo ni hasara isiyoweza kubadilishwa.”

Hiki ni kiwango cha juu kabisa kwenye orodha rasmi duniani, ingawa shirika la afya duniani –WHO inaamini kwamba idadi ya kweli ya vifo inaweza kuwa kubwa zaidi kwingineko. Marekani pia imerekodi watu milioni 80 waloambukizwa Covid kati ya watu milioni 330. Kesi ya kwanza iliyothibitishwa ilikuwa januari 20 mwaka 2020 wakati mtu mmoja aliposafiri kwa ndege kwenda Seattle kutoka WUHAN China. Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 35 alinusurika baada ya kuugua homa ya mapafu kwa siku kumi , kukohoa , homa kichefuchefu pamoja na kutapika. Lakini vifo vilianza kuripotiwa wiki chache baadae. Tangu miaka miwili iliyopita, viwango vya vifo vimepungua kuendana na mawimbi ya virusi yanavyoendea kote nchini na kufikia kiwango cha juu cha zaidi ya 4,000 kwa siku mapema mwaka 2021.