Greta Thunberg siku ya Alhamisi ameitaka sekta ya nishati duniani na wafadhili wake kuacha kuwekeza katika mafuta ghafi ya fossil katika mkutano wa ngazi ya juu huko Davos na mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA)
Wakati wa majadiliano na Fatih Birol pembeni ya mkutano wa kila mwaka wa Jukwaa la Kiuchumi la Kimataifa (WEF), wanaharakati walisema wamewasilisha barua kwa mtendaji mkuu yenye ujumbe wa “sitisha na kujiepusha” wakitaka kusimamishwa kwa uchimbaji mpya wa mafuta, gesi na makaa ya mawe.
“Kadiri watakavyoweza kujipurukusha kwa hilo, wataendelea kuwekeza katika mafuta ya fossil, wataendelea kuwaangamiza watu,” Thunberg alionya.
Sekta ya mafuta na gesi, ambayo imetuhumiwa na wanaharakati kwa kuteka mjadala wa mabadiliko ya hali ya hewa huko katika eneo la mapumziko nchini Uswizi, imesema inapaswa wawe ni sehemu ya kipindi cha mpito cha nishati wakati mafuta ya fossil yataendelea kuwa na mchango mkubwa katika mchanganyiko wa nishati wakati dunia ikihamia katika uchumi wenye kiwango kidogo cha carbon.
Thunberg, ambaye alizuiliwa na polisi wa Ujerumani wiki hii wakati wa maandamano kwenye mgodi wa makaa ya mawe, aliungana na wanaharakati wenzake Helena Gualinga kutoka Ecuador, Vanessa Nakate kutoka Uganda, na Luisa Neubauer kutoka Ujerumani kujadili njia ya kutatua masuala makubwa na Birol.
Birol, ambaye shirika lake linaandaa mapendekezo ya sera ya nishati, aliwashukuru wanaharakati kwa kukutana naye, lakini alisisitiza kuwa suala la mpito lazima lijumuishe mchanganyiko wa wadau, hususan wakati huu wa dunia inapokabiliwa na mgogoro wa usalama wa nishati.
Mkuu wa IEA, ambaye mapema Alhamisi alikutana na baadhi ya watu maarufu katika sekta ya mafuta na gesi huko Davos, alisema hakuna sababu ya kuhalalisha uwekezaji katika vitalu vipya vya mafuta kwa sababu ya uhaba wa nishati, akisema kuwa wakati uwekezaji huu ukianza kutumika mgogoro wa hali ya hewa utakuwa umefikia hali mbaya zaidi.
Pia alisema hakuwa amekata tamaa kuliko wanaharakati wa hali ya hewa kuhusu hatua ya kuhamia katika nishati salama.
“Tunaweza kuwa na haki ya kuwa na matumaini kidogo,” alisema, akiongeza: “Mwaka jana kiwango cha nishati mbadala zilizokuwa zinakuja katika soko zilikuwa katika rekodi ya juu.”
Lakini alikiri kuwa hatua hii ya mpito haijafanyika kwa haraka na kuonya kuwa nchi zinazoendelea na kukua ziko hatarini kuachwa nyuma iwapo uchumi uliokuwa mkubwa hautazisaidia katika hatua hii ya mpito.
Chanzo cha habari hii ni Reuters.