Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 21:22

Barua ya Trump inayosifu Waafrika yazua hisia mseto


Rais wa Guinea Alpha Conde azungumza na katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Antonio Guterres. Addis Ababa,Ethiopia. Jan. 28, 2018.
Rais wa Guinea Alpha Conde azungumza na katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Antonio Guterres. Addis Ababa,Ethiopia. Jan. 28, 2018.

Barua iliyoandikwa na rais Donald Trump, ikisifu ushirikiano kati ya Marekani na mataifa ya Afrika, ilipokelewa kwa mseto wa hisia kati ya viongozi wa bara hilo wanaohudhuria mkutano wa 30 mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Trump alisema kama ishara kwamba anaiheshimu Afrika, atamtuma waziri wake wa mambo ya nje, Rex Tillerson kutembelea mataifa kadhaa kuanzia mwezi Machi mwaka huu.

Alisema kwamba White House itawaalika viongozi kadhaa kutoka bara la Afrika katika juhudi za kuimarisha uhusiano huo.

"Marekani ina heshima kuu kwa mataifa ya Afrika na raia wake," barua hiyo ilisema.

"Wanajeshi wetu wanapigana kwa pamoja na wale wa Afrika," iliendelea kueleza.

Haya yanajiri huku baadhi ya viongozi wakiendelea kumshutumu rais Trump, kufuatia kuibuka kwa ripoti kwamba alitumia maneno ya kudhalilisha dhidi ya wahamiaji kutoka bara la Afrika na nchi ya Haiti.

Hata hivyo, Trump amekanusha madai hayo.

Katika mahojiano ya moja kwa moja na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika, waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Augustine Mahiga, alisema nchi yake inaikaribisha barua hiyo, na kusema kwamba inaonekana rais huyo ameungama "dhambi zake" na kuomba msamaha.

"Hii ni mara ya kwanza kwa rais wa Marekani kutumia maneno yaliyo na ushawishi kwamba anamaanisha anachokisema," alisema balozi Mahiga.

Ijuamaa, Rais Trump alikutana na rais wa Rwanda, Paul Kagame, kwenye mji wa Davos, Uswizi, na kumsifu kama "rafiki."

Kagame pia ndiye mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika.

Wakati huo huo, Katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Antonio Guterres, Jumapili aliahidi kushirikiana zaidi na bara la Afrika na kusema kwamba Umoja huo utatoa usaidizi zaidi kwa ajili ya kuimarisha usalama.

Guterres alikuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha marais na vingozi wa serikali wanachama wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia.

"Ninaamini kwa dhati kwamba bara la Afrika ni tegemeo muhimu sana duniani," alisema.

Alisema Umoja wa Mataifa utaongeza ufadhili kwa vikosi vya kulinda usalama katika mataifa kama vile Somalia, Nigeria na nchi zingine za bara hilo.

Mkutano huo wa 30 unatarajiwa kujibu barua iliyoandikwa na rais Trump kufuatia tuhuma kwamba alitumia maneno ya kudhalilisha yaliyowalenga wahamiaji kutoka mataifa ya Kiafrika pamoja na wale wa kutoka Haiti.

Tayari Umoja wa Afrika, kupitia balozi wake Mmarekani, ulituma ujumbe wa kuelezea kutoridhishwa na madai hayo.

XS
SM
MD
LG