Maeneo machache yaripotiwa kuwa na ghasia Kenya

Rais Uhuru Kenyatta

Masaa kadhaa baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Kenya kumtangaza Rais mteule Uhuru Kenyatta mshindi katika uchaguzi wa 2017 kumekuwa na uvunjifu wa amani katika baadhi ya maeneo nchini Kenya.

Maeneo hayo ni Nyanza na baadhi ya vitongoji vya Nairobi ambapo kulikuwa na vurugu, uharibifu wa mali na vifo vilivyoripotiwa.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Kenya polisi wamekuwa wakipambana na waandamanaji katika maeneo ya Kisumu, Mathare na Kibera. Inahofiwa kuwa watu sita wamepoteza maisha kutoka na majeraha ya risasi usiku wa Ijumaa.

Habari nyingine zimesema kuwa polisi katika maeneo ya Kisumu, Siaya, Bondo, Homa Bay na Migori wameendelea kupambana na makundi mbalimbali. Barabara zimefungwa na biashara kuchomwa moto.

Kwa mujibu wa waandishi wa habari wa KTN Jumamosi walitembelea eneo la Kibera na kusikia milio ya risasi. Njia zote kuu katika maeneo mengi ya Nyanza hazipitiki wakati watu wakiwa majumbani wamejifungia. Polisi wamethibitisha kuwa Mtu mmoja aliuawa.