Ethiopia kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa

Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn

Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn ametangaza Jumatano kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa na kufungwa kwa vituo vinavyojulikana kwa mateso katika kile alichokiita kuwa ni juhudi ya nchi hiyo “kupanua wigo wa demokrasia kwa watu wote.”

Ethiopia imekuwa ikituhumiwa kwa kukandamiza haki za binadamu, ikiwemo ukamataji wa watu holela ili kuzuia upinzani na kuwatesa wafungwa katika kizuizi maarufu cha Maekelawi kilichoko mji mkuu wa Addis Ababa.

Katika hatua ya kushangaza iliyochukuliwa na serikali, Hailemariam amewaambia waandishi wa habari kuwa makosa yote ya wafungwa hao yatafutwa – ambao siku za nyuma walikuwa wanatuhumiwa kama wahalifu bila maelezo yoyote – ambao walikuwa wanasubiri hukumu.

“Wafungwa wa kisiasa ambao wanakabiliwa na kesi na tayari wamekamatwa wataachiliwa huru,” Hailemariam amesema “na Jela maarufu kwa mateso ya ambayo inajulikana kama Maekelawi itafungwa na kufanya ni jumba la kumbukumbu.”

Hata hivyo hakujulikana mara moja ni wafungwa wangapi walikuwa wanashikiliwa katika kituo hicho, ambacho shirika la Human Rights Watch linalotetea haki za binadamu lilitoa ripoti mwaka 2013, ikidai kuwa “njia haramu za kusaili wafungwa” zimekuwa zikitumika dhidi ya wafungwa.

Taasisi zote mbili za kimataifa zinazoshughulikia haki za binadamu; Human Rights Watch na Amnesty international wameishutumu Ethiopia kwa kuwakamata watu kiholela, kuwatesa na kuendesha mashtaka bila uadilifu dhidi ya wapinzani wa vyama vya kisiasa.

Tangazo hilo la Hailemariam limekuja baada ya maandamano kadhaa dhidi ya serikali miezi ya karibuni nchini Ethiopia katika mikoa yenye machafuko ya Oromia na Amhara. Maandamano hayo yalienea nchi nzima, ambapo ilipelekea serikali kutangaza hali ya hatari ambayo imeondolewa.