Jeshi la Misri limevunja bunge na kusimamisha matumizi ya katiba, wakikidhi madai makuu mawili ya waandamanaji wanaounga demokrasia baada ya siku 18 za ghasia ambazo zilimtoa madarakani Rais Hosni Mubarak.
Utawala wa kijeshi ambao ulichukua udhibiti wakati bwana Mubarak alipojiuzulu Ijumaa, ulitoa taarifa Jumapili ukisema utaongoza kwa muda wa miezi sita au hadi uchaguzi wa Rais na bunge utakapofanyika. Uchaguzi kwa sasa umepangwa kufanyia mwezi Septemba.
Taarifa ilitolewa muda mfupi baada ya Waziri Mkuu wa Misri, Ahmed Shafiq, aliposema kipaumbele cha baraza lake la mawazili linaloungwa mkono na jeshi ni kurejesha usalama na maisha ya kawaida huko Misri. Pia alisema nyadhifa kadhaa katika baraza la mawaziri zinabaki wazi na aliahidi kwamba uteuzi wowote mpya utakuwa unakubalika na jamii.
Mkutano huo na waandishi wa habari ulikuwa mkutano wa kwanza wa Waziri Mkuu tangu bwana Mubarak alipojiuzulu Ijumaa na kukabidhi madaraka kwa jeshi kufuatia shinikizo la waandamanaji wengi dhidi ya utawala wake wa takribani miaka 30. Bwana Mubarak alimteuwa bwana Shafiq kama Waziri Mkuu Januari 29, siku nne baada ya maandamano kuanza.