ECOWAS katika hatari ya kusambaratika baada ya Mali, Niger na Burkina Faso kuunda shirikisho lao

Watawala wa kijesi wa Niger, Mali na Burkina Faso wakikutana mjini Niamey, Niger, Julai 6, 2024. Picha ya Reuters

Jumuia ya uchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS Jumapili ilionya kwamba kanda hiyo inakabiliwa na “kusambaratika” baada ya watawala wa kijeshi wa Niger, Mali na Burkina Faso kusisitiza msimamo wao wa kutaka jumuia hiyo ivunjwe.

Nchi hizo tatu ziliunda “shirikisho la mataifa ya Sahel” kwenye mkutano wao mkesha wa mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa ECOWAS, na kuashiria mtihani mwingine kwa Jumuia hiyo ambayo watawala hao wa kijeshi walitangaza kujitenga nao mapema mwaka huu.

ECOWAS tayari inapambana na ghasia mbaya za makundi ya wanajihadi, matatizo ya kifedha na changamoto za kuimarisha jeshi la kikanda.

Haikufamika wazi ni hatua gani jumuia hiyo itachukua baada ya mkutano wake katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja.

Lakini mwenyekiti wa tume ya ECOWAS, Omar Alieu Touray, alisema kujiondoa kwa nchi za Sahel kuna hatari ya “kutengwa kisiasa”, kupoteza mamilioni ya dola katika ufadhili na kukwamisha uhuru wa usafiri.

Kuvunjika kwa jumuia hiyo kutazidisha ukosefu wa usalama na kudhoofisha kazi ya kikosi cha kikanda kilichopendekezwa kwa muda mrefu, Touray alisema.

“Kanda yetu inakabiliwa na hatari ya kusambaratika,” alionya.