Afisa mmoja wa timu ya kukabiliana na virusi hivyo amesema hayo, akiongeza kwamba kampeni ya kusambaza chanjo itachukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa.
Mchakato wa chanjo ya mpox nchini Kongo ulizinduliwa mwezi huu katika eneo la mashariki lililoathirika zaidi.
Mwandishi wa Reuters aliyetembelea kituo cha utoaji chanjo katika jimbo la Kivu Kaskazini alisema kuwa wenyeji walionekana kutofahamu au walikuwa na mashaka kuhusu chanjo hizo.
Cris Kacita, mkuu wa timu ya kukabiliana na mpox Kongo, alisema mengi zaidi yanahitaji kufanywa ili kuongeza idadi ya watu waliopatiwa chanjo, akiongeza kuwa kampeni inayoendelea ya chanjo itachukua muda mrefu, zaidi ya siku 10 zilizopangwa.
"Kampeni ya uhamasishaji imefanywa, lakini kwa kiwango cha chini tu. Haya ni mapengo ambayo yanahitaji kuzibwa," aliliambia shirika la habari la Reuters.
Wakati wa ziara ya hivi karibuni katika kituo cha chanjo huko Kibati, kambi inayohifadhi watu waliokimbia makazi yao katika jimbo la Kivu Kaskazini, wakazi walielezea kutopokea taarifa zozote kuhusu juhudi za utoaji chanjo.
Kampeni ya chanjo ya mpox nchini Kongo ni hatua muhimu katika juhudi za kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo katika kitovu chake, ambapo umeenea katika mataifa mengine mengi ya Afrika mwaka huu.