Msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema kuwa maafisa wake wametangaza mlipuko wa Ebola katika eneo la jimbo la Bas-Uele baada ya uchunguzi wa maabara kuthibitisha kuwepo kwa ugonjwa huo.
Msemaji wake, Christian Lindmeier, ameiambia VOA kwamba watu tisa katika eneo hilo wanaugua na imeelezwa kuwa ni homa ya Ebola.
Habari hizo zimeeleza kuwa watu watatu tayari wamefariki dunia.
WHO imesema kwenye akaunti ya Twitter kuwa inashirikiana na Wizara ya Afya ya Congo katika kudhibiti mripuko huo.
Wizara imesema katika tamko lake kwamba timu za madaktari, waratibu na wataalamu wameelekea katika eneo hilo na watawasili huko Jumamosi.
Mripuko wa ugonjwa wa Ebola mara ya mwisho ulitokea Kongo mwaka 2014 na kuua zaidi ya watu 40.
Ugonjwa huo ulizuka tena na kuathiri eneo kubwa la Guinea, Liberia na Sierra Leone mwaka huo na kuua watu zaidi ya 11,000.