Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 20:43

Tanzania, Afrika Kusini zaingia katika ushirikiano wa kihistoria


Rais John Magufuli (K) akiwa na Rais Jacob Zuma, Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu mstaafu Salim Ahmed Salim
Rais John Magufuli (K) akiwa na Rais Jacob Zuma, Rais mstaafu Benjamin Mkapa na Waziri Mkuu mstaafu Salim Ahmed Salim

NCHI za Tanzania na Afrika Kusini zimekubaliana kushirikiana katika maeneo 11 yakiwamo ya biashara, uwekezaji, afya, elimu, sayansi, teknolojia, uchumi wa viwanda, ulinzi na usalama, utalii na madini ambayo yataisaidia Tanzania kukuza uchumi wake.

Nchi hizo mbili zimekubaliana kuondoa vikwazo vyote ambavyo vinakwamisha biashara kati yake.

Aidha katika eneo la uchumi wa viwanda, nchi hizo zimekubaliana kupitia mkakati wa Maendeleo ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), kuhamasisha uwekezaji nchini katika maeneo mbalimbali ikiwemo mifugo, madini na kilimo ili kuinua sekta ya viwanda.

Mazungumzo ya ndani

Rais John Magufuli katika mazungumzo ya ndani na Rais Jacob Zuma alimweleza kuhusu azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kutaka Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Akizungumzia eneo la ujenzi wa miundombinu, usafiri na nishati, alisema

Nchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika kutekeleza miradi mbalimbali zikiwemo ujenzi wa miundombinu, usafiri na nishati.

Hata hivyo Tanzania tayari imewasilisha ombi la wawekezaji kutoka Afrika Kusini kujitokeza kwa wingi na kuwekeza katika miradi iliyopo ikiwemo mradi wa treni ya kisasa ya standard gauge na makaa ya mawe.

Rais Magufuli alitumia fursa hiyo kumuomba Rais Zuma ambaye nchi yake ni mwanachama wa nchi tano zenye nguvu kiuchumi zikiwemo Brazil, Urusi, China na India (Brics), kwa ajili ya kuiombea Tanzania mkopo nafuu na kumalizia mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa ya standard Gauge kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.

Harakati za ukombozi

“Ni ukweli kuwa Tanzania tumefanya mengi katika ukombozi wa nchi za Afrika, tumejitolea katika mambo mengi na kwa upendo mkubwa. Ndio maana tunaomba hawa tuliowasaidia nao watusaidia kidogo. Nashukuru kwani katika hili tayari Rais Zuma ameonesha nia ya kutusaidia,” alisisitiza Dk Magufuli.

Aidha katika eneo la utalii nchi hizo zimekubaliana kushirikiana na kubadilishana uzoefu na utalaamu hususani katika kutoa huduma za kitalii.

“Lakini pia tumeomba wawekezaji kutoka Afrika Kusini waje wawekeze kwenye ujenzi wa hoteli na kuboresha fukwe kwani kwa sasa Tanzania imebarikiwa kuwa na fukwe nyingi ambazo hazijaendelezwa,” alieleza Dk Magufuli.

Kuhamasisha wawekezaji

Jambo jingine muhimu lililofikiwa katika ziara hiyo ni makubaliano ya kushirikiana katika kubadilishana uzoefu, utaalamu na usimamizi ikiwemo kuwahamasisha wawekezaji wa Afrika Kusini kutumia fursa hiyo na kuwekeza katika viwanda vya kuchakatua michanga ya dhahabu hapa nchini badala ya kupelekwa nje ya nchi.

Pianchi hizo zimekubaliana kushirikiana katika eneo la afya kutokana na ukweli kuwa nchi ya Afrika Kusini imepigahatua hasa katika eneo la tiba ya magonjwa ya moyo na figo.

Kupitia makubaliano hayo, Tanzania imeomba uwekezaji kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya dawa.

Akielezea eneo la elimu, sayansi na teknolojia, Dk Magufuli lisema nchi hizo zimekubaliana kushirikiana kupitia eneo la utafiti na elimu ya juu kwa kubadilisha uzoefu wa walimu lakini pia Tanzania imekubali kupeleka walimu wa Kiswahili kwenda kufundisha Afrika Kusini.

Alisema pia wamekubaliana kushirikiana katika ulinzi na usalama katika kupambana na uhalifu wa ugaidi, biashara ya binadamu, uharamia, ujangili na dawa za kulevya.

Pamoja na hayo, alibainisha kuwa nchi hizo mbili zimekubaliana kuendelea kushirikiana kupitia vyama vyao vya siasa vikongwe vya ANC na CCM ambavyo vina historia ndefu Afrika.

Utatuzi wa migogoro

Marais hao wamekubaliana kuhakikisha wanashirikiana katika kutatua migogoro ya nchi nyingine za Afrika hasa migogoro inayoendelea katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Lesotho.

Nchi hizo mbili zimefikia makubaliano hayo na mikataba ya ushirikiano ambayo nchi hizo tayari imeingia yanatekelezwa ipasavyo, wamekubaliana kuunda chombo cha usimamizi kitakachofuatilia utekelezaji wa makubaliano na mikataba hiyo na endapo kutabainika kikwazo au uzembe hatua zichukulie kudhibiti.

“Napenda Watanzania watambue kuwa ziara hii ina mafanikio makubwa sana, Afrika Kusini ni ndugu zetu nawahakikishia Tanzania itaendelea kuheshimu uhusiano uliopo kwa manufaa ya wananchi wetu,” alisema Dk Magufuli.

Mawaziri wa mambo ya nje

Kwa upande wake, Rais Zuma alizungumzia mazungumzo yake na mwenyeji wake na kubainisha kuwa wamekubaliana kuyaunga mkono mapendekezo ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili yaliyowasilishwa na mawaziri wote wawili wa Tanzania na Afrika Kusini.

Alisema katika mazungumzo hayo wamekubaliana mambo mengi ikiwemo kushirikiana katika ulinzi na usalama, elimu, sayansi na teknolojia, biashara na uwekezaji, uchukuzi, nishati na madini.

“Lakini kikubwa zaidi tumekubaliana kukuza uchumi wetu kwa kushirikiana na sekta binafsi,” amesema Rais Zuma.

Vyanzo vya habari vimesema nchini Tanzania kwamba ziara yake hiyo ni ya mafanikio kwani pamoja na mambo mengine wamezindua Tume ya Marais ambayo kazi yake kubwa itakuwa ni kusimamia ukuaji wa uhusiano baina ya nchi hizo mbili na wamepanga tume hiyo kukutana mara kadhaa tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambako tangu iundwe mwaka 2011, imekutana kwa mara ya kwanza mwaka huu.

XS
SM
MD
LG