Dozi 100,000 za chanjo dhidi ya Mpox zatarajiwa nchini DRC leo Alhamisi

Wagonjwa wakimsikiliza daktari nje ya kituo kinachotoa matibabu ya Mpox huko Goma Kaskazini, DRC Agosti 17, 2024. Picha na AFP

Shehena ya kwanza ya dozi 100,000 za chanjo ya mpox itawasili nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Alhamisi, kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa barani Afrika kimesema, huku jumla ya chanjo 200,000 zikitarajiwa wiki hii.

Nchi hiyo kubwa ya Afrika ya Kati yenye watu milioni 100 ni kitovu cha mlipuko wa mpox, ambako visa na vifo vinazidi kuongezeka.

“Tumefurahishwa sana na kuwasili kwa shehena hii ya kwanza ya chanjo nchini DRC, Jean Kaseya, mkuu wa kituo cha Afrika cha kudhibiti na kuzuia magonjwa, aliiambia AFP, akiongeza kuwa zaidi ya dozi 99,000 zilitarajiwa leo Alhamisi.

Zaidi ya visa 17,500 na vifo 629 vimeripotiwa nchini humo tangu mwanzoni mwa mwaka huu, kulingana na shirika la afya duniani (WHO).

Ndege ya kwanza ya mizigo ikibeba dozi hizo za chanjo ya mpox iliondoka Jumatano jioni katika mji mkuu wa Denmark, Copenhagen na inatarajiwa kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa mjini Kinshasa saa saba mchana saa za huko.

Ndege nyingine inayobeba chanjo zinazosalia imepangwa kuwasili kabla ya mwisho wa wiki hii, CDC Afrika imethibitisha.

Chanjo hizo za kwanza ni kutoka maabara ya kampuni ya kutengeneza dawa ya Denmark, Bavarian Nordic.

Kulingana na WHO, serikali ya DRC inapanga kuanza kutoa chanjo hizo mwishoni mwa juma.