Djibouti: Uchaguzi wa wabunge Ijumaa kususiwa na upinzani

Mpiga kura wa Djibouti katika uchaguzi wa awali

Raia wa Djibouti watapiga kura kesho Ijumaa katika uchaguzi wa wabunge, uliosusiwa na vyama vikuu vya upinzani, ambavyo vinadai kura hiyo imegubikwa na udanganyifu.

Ni vyama viwili pekee vinavyogombea viti katika Bunge la Kitaifa lenye wabunge 65, ambapo chama tawala cha Rais mkongwe Ismael Omar Guelleh cha Union for Presidential Majority (UMP), kinatarajiwa kupata ushindi.

Licha ya kuwa taifa dogo, Djibouti ina nafasi muhimu ya kimkakati kwa sababu ya uwepo wake kwenye pwani ya bahari ya sham, ikiitumia kuwavutia wawekezaji, na mataifa yenye nguvu za kijeshi.

Upinzani una wasiwasi kuwa uchaguzi huo, ambao unafuatia kura ya urais mwezi Aprili 2021, ambayo ilimfanya Guelleh kuchaguliwa tena kwa muhula wa tano kwa asilimia 97 ya kura, hautakuwa huru na wa haki.

Guelleh, mwenye umri wa miaka 75, ameitawala Djibouti kwa kutumia nguvu tangu 1999 na nchi hiyo imeshuhudia kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari na kukandamiza upinzani.

Uchumi wa Djibouti ulipata pigo mwaka 2022 kutokana na vita vya Ukraine, ukame, na mzozo wa miaka miwili katika nchi jirani ya Ethiopia, lakini unatarajiwa kukua kwa karibu asilimia tano mwaka huu, kulingana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).