Onyo hilo linatolewa wakati madhehebu ya dini yakieleza hali ilivyo katika taasisi zao kuhusiana na janga hilo ambalo linaendelea kuisumbua dunia.
Msemaji Mkuu wa serikali Hassan Abbas amesema ni kinyume cha taratibu mtu kutoa taarifa zinazohusiana na majanga kama vile mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona.
“Serikali imeweka utaratibu ambao unabainisha wazi ni nani mwenye mamlaka ya kutoa taarifa za namna hiyo.
Ameeleza serikali imelazimika kujitokeza kufafanua jambo hilo hasa baada ya kuendelea kushuhudia mwenendo mpya aliouita “kwa baadhi ya watu kutumia njia mbalimbali kusambaza taarifa ambazo haziko ndani ya mamlaka yao.”
Tangu mwaka 2020 hakuna takwimu zozote zilizotolewa na serikali kuhusiana na idadi ya waliokumbwa na janga hilo wala wale waliopoteza maisha.
Hata hivyo vyanzo vya habari vinasema serikali hiyo imeendelea kusisitiza kuwa inaamini iko katika mkondo sahihi katika kukabiliana na ugonjwa huo wa COVID-19.
Serikali inasema inaendelea kuchukua tahadhari zote kukabiliana na janga hilo na kuwa hadi wakati huu janga hilo ambalo linaendelea kuwa ni tishio kubwa duniani limedhibitiwa vya kutosha nchini Tanzania.
Vyanzo hivyo vya habari vinaesema msemaji huyo wa serikali hakuweka bayana ni kina nani ambao wamekuwa wakitoa takwimu na taarifa kuhusiana na maambukizi ya janga hilo, hata hivyo hivi karibuni baadhi ya makanisa yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara kuzungumzia janga hilo.
Kanisa Katoliki ndilo lililokwenda mbali zaidi kwa kuweka mwongozo unaopaswa kufuatwa na waaumini wake wakati wanaposhiriki ibada makanisani na namna watakavyoadhimisha sikukuu ya Pasaka.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu, Padre Charles Kitima alielezea wiki hii jinsi kanisa hilo linavyokumbwa na majonzi baada ya kupoteza makasisi wake 25 katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kutokana na matatizo yaliyoambatana na upumuaji.