Comoros yapiga kura kuwachagua wabunge

Wapiga kura wakitizama orodha ya wapiga kura kwenye kituo cha kuoigia kura huko Mitsoudje, Januari 12, 2025. Picha ya AFP

Comoros Jumapili ilipiga kura kuwachagua wabunge, huku makundi mengi ya upinzani yakisema yatasusia uchaguzi huo ambao wanadai hauna uwazi.

Mtoto mkubwa wa Rais wa Comoros Azali Assoumani, Nour El Fath Azali, mwenye umri wa miaka 39 na katibu mkuu wa serikali amegombea kuwakilisha eneo bunge nje kidogo ya mji mkuu Moroni.

Vituo vingi vya kupigia kura vilichelewa kufunguliwa baada ya vifaa vya kupigia kura kushindwa kufikishwa mapema katika muda rasmi wa saa moja asubuhi, mwandishi wa habari wa AFP alishuhudia.

Zoezi la kupiga kura lilitarajiwa kumalizika saa 10 alasiri, lakini upigaji kura ulimalizika saa mbili baadaye kutokana na zoezi hilo kuanza kwa kuchelewa na hali mbaya ya hewa.

Kabla ya kuteuliwa kwenye wadhifa wake mwezi Julai mwaka jana, Nour alikuwa mshauri wa baba yake, mwenye umri wa miaka 65, mwanajeshi wa zamani ambaye aliingia madarakani katika mapinduzi ya mwaka 1999.

Wakosoaji wamesema majukumu mapya ya Nour, ambayo ni pamoja na kuidhinisha amri zote zinazotolewa na mawaziri na magavana, yameinua jukumu lake kwenye cheo cha waziri mkuu.

Azali alichaguliwa kwa muhula mwingine mwezi Januari mwaka 2024 baada ya uchaguzi wenye utata uliofuatiwa na maandamano mabaya ya siku mbili. Ameshtumiwa kwa kuongoza nchi kimabavu.