Comey aliomba raslimali zaidi kuichunguza Russia - Wabunge

Mwanasheria Mkuu Jeff Sessions

Maafisa wa Bunge la Marekani wamesema kuwa mkurugenzi wa FBI aliyefukuzwa kazi James Comey siku chache kabla ya kuondolewa madarakani alikuwa ameomba fedha zaidi kwa ajili ya kuichunguza Russia.

FBI ilikuwa imeanza kufanya uchunguzi juu ya kuhusika kwa Russia kuvuruga uchaguzi wa Marekani mwaka jana na kuwepo uwezekano wa mafungamano kati ya Russia na Kampeni ya Rais Donald Trump.

Maafisa hao wamesema kuwa ombi hilo alilipeleka kwa naibu Mwanasheria Mkuu Rod Rosenstein, ambaye pamoja na Mwanasheria Mkuu Jeff Sessions waliainisha katika nyaraka zao Jumanne sababu zilizopelekea uongozi kumuondoa Comey madarakani.

Idara ya Sheria imekanusha kwamba kulikuwa na maombi yoyote kutoka kwa Comey. Matokeo na athari zake, kama zipo, kutokana na ombi hilo haziko wazi iwapo ombi hilo lilipelekea uamuzi wa Trump kumfukuza Comey.

Sababu za Comey kufukuzwa zilikuwa zimeainishwa katika barua mbili zilizokuwa zimeandikwa na Sessions na Rosenstein. Kimsingi zilikuwa zinamtuhumu Comey kwa kuchukua sheria mikononi mwake.

Gazeti la Washington Post, lilitaja chanzo cha habari bila ya kutaja jina, kimeelezea mapema Alhamisi kuwa Rosenstein alikuwa ametishia kujiuzulu alipogundua kuwa White House ilikuwa imemuelezea kama ndiye mtu aliyekuwa sababu ya kufukuzwa kazi Comey na kuwa rais alikuwa anafuata mapendekezo yake katika uamuzi huo.

Waliokerwa na kufukuzwa kwa mkurugenzi wa FBI wanasema kuwa inazidi kuleta maswali zaidi kuhusu uchunguzi uliokuwa unafanywa na FBI.

Wapelelezi wa siku nyingi FBI na wengine walioko Idara ya Sheria “wataendelea kuwa na hamu kuona suala hili linasonga mbele kwa kiwango cha kupatikana ushahidi wa makosa yoyote, aina yoyote ya mahusiano na kuhusika kwa Russia,” amesema mstaafu Mwanasheria Mkuu Alberto Gonzalez ameiambia VOA.