Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi na mwenzake wa Nauru Lionel Aingimea, walisaini nyaraka rasmi katika tafrija iliyofanyika katika Nyumba ya Wageni huko Diaoyutai, mjini Beijing.
Sherehe hizo zilikamilisha kwa haraka mtiririko wa matukio yalioanza Januari 15 wakati Nauru ilipotangaza ilikuwa ikibadilisha mahusiano yake kutoka Taiwan kwenda China.
Tangazo hilo lilikuja siku mbili baada ya Makamu Rais wa Taiwan Lai Ching-te, wa Chama kinacho unga mkono demokrasia cha Democratic Progressive, alipochaguliwa kuwa rais ajaye wa kisiwa hicho.
Nauru imekuwa ikibadilisha badilisha msimamo wake kati ya kuiunga mkono China na Taiwan tangu mwaka 1980, ambapo hapo awali iliitambua Taiwan.
Taifa hilo dogo la kisiwani liliitambua Beijing mwaka 2002, na baadaye kurejesha uhusiano wake na Taipei miaka mitatu baadaye.
Mabadiliko hayo yanaonyesha ushindi mwingine ikiwa ni lengo la China la kuitenga Taiwan kutoka katika jumuiya ya kimataifa, ikiwemo kuwashawishi washirika wa Taiwan kuhamisha ushirikiano wao kwa China.
Beijing inakichukulia kisiwa hicho ni jimbo lililojitenga na imeapa kuirejesha Taiwan chini ya himaya yake kwa namna yoyote ile, ikiwemo kutumia nguvu za kijeshi.
Taiwan kumpoteza mshirika wake Nauru imemuacha na washirika wa kidiplomasia 12, ikiwemo Guatemala huko Amerika ya Kati, taifa la Amerika Kusini la Paraguay, nchi za Pacific za Palau, Tuvalu na visiwa vya Marshall, na Vatican.
Ripoti ya mwandishi wa VOA Richard Green.