Bunge jipya linatarajiwa kukutana kwa mara ya kwanza mjini Cape Town Ijumaa baada ya matokeo ya uchaguzi kuonyesha kuwa hakuna chama kilichopata ushindi wa kutosha.
Chama cha IFP kilipata viti 17 katika bunge la taifa lenye viti 400 ambapo wabunge wataitishwa kumteua spika na kumchagua rais wa nchi.
ANC, kikiwa na viti 159, tayari kimeashiria kuwa kinataka serikali ya umoja wa kitaifa yenye kundi kubwa la vyama, kuanzia mrengo wa kulia hadi mrengo mkali wa kushoto.
“Ni wakati kwa IFP kuiimarisha serikali tena,” kiongozi wa chama Velenkosini Hlabisa aliuambia mkutano wa waandishi wa habari.
“Tunaweka mbele uthabiti na maslahi ya Afrika Kusini, kama tulivyoahidi kufanya wakati wa kampeni ya uchaguzi,” alisema.
Ameongeza kuwa “Katika serikali mpya, chama cha IFP kitaleta uadilifu, na msukumo wa kuendeleza nchi yetu na wananchi wetu kuelekea mustakabali bora.”
Vyama vya kisiasa vimekuwa vikijitahidi kujenga muungano baada ya chama cha African National Congress cha Rais Cyril Ramaphosa kupoteza wingi wa kura kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa Mei 29.
Chama hicho kilipata asimilia 40 ya kura, ushindi wake mdogo kuwahi kupata, na sasa kinahitaji kuungwa mkono na vyama vingine ili kiweze kutawala.