Taifa hilo la Afrika Mashariki limekuwa likishuhudia mvua kubwa katika wiki za hivi karibuni ambazo zimesababisha vifo vya watu 58 nchini Tanzania katika nusu ya kwanza ya mwezi Aprili, na watu 13 nchini Kenya.
Burundi ambayo Umoja wa mataifa unasema ni moja ya nchi 20 zilizo katika hatari kubwa ya kukabiliwa na mabadiliko ya hali ya hewa, imekumbwa na mvua zinazonyesha karibu kila siku tangu mwezi Septemba, huku mji mkuu Bujumbura ukiharibiwa na mafuriko.
“Mvua kubwa zinanyesha kutokana na upepo wa baharini wa El Nino unaosababisha mafuriko makubwa yanayohusishwa na mito kufurika na kuongezeka kwa maji ya Ziwa Tanganyika.
Maporomoko ya ardhi, upepo mkali na mvua ya barafu vinaendelea kuhatarisha jamii na kuziweka katika mazingira magumu tofauti,” waziri wa mambo ya ndani Martin Niteretse na mratibu wa misaada wa Umoja wa mataifa Violet Kenyana Kakyomya walisema katika taarifa ya pamoja jana Jumanne.
Kati ya Septemba na Aprili 7, jumla ya watu 203,994 waliathirika huku idadi ya waliohama makazi yao ikiongezeka kwa asilimia 25 hadi watu 96,000, walisema.