Burkina Faso, Niger na Mali zitaunda “kikosi cha pamoja ” ndani ya wiki chache, waziri wa ulinzi wa Niger alisema.
Mataifa hayo matatu ni makoloni ya zamani ya Ufaransa ambako wanajeshi waliondoa tawala za kiraia katika mapinduzi kati ya mwaka 2020 na 2023.
Kufuatia mapinduzi hayo, nchi hizo tatu zilijitenga na Ufaransa na mwaka jana ziliunda shirikisho, the Alliance of Sahel States (AES).
“Katika eneo hili la pamoja, majeshi yetu yataweza kuingilia kati kwa pamoja,” waziri wa ulinzi wa Niger, Salifou Mody alisema katika mahojiano ya televisheni, akiongeza kuwa kikosi cha wanajeshi 5,000 “kiko tayari”.
“Kikosi hiki cha pamoja hakitakuwa tu na wanajeshi, bali pia na vifaa vya anga, ardhini na kijasusi pamoja na mfumo wa uratibu”, alisema, akiongeza kwamba kitaanza kufanya kazi ndani ya wiki chache.
Zikichukuliwa pamoja, nchi hizo tatu zimetawanyika katika eneo la zaidi ya kilomita mraba milioni 2.8, ikiwa mara nne ya ukubwa wa Ufaransa, kaskazini magharibi mwa Afrika.